Pata taarifa kuu

Rishi Sunak nchini Poland kutangaza msaada mpya wa kijeshi kwa Ukraine

Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak amewasili Poland siku ya Jumanne, ambapo atatangaza nyongeza ya pauni milioni 500 kama msaada na usambazaji wa silaha mpya kwa Ukraine, ambayo inakabiliwa na "tishio lililopo", Downing Street imetangaza.

Waziri Mkuu Rishi Sunak azungumza na Rais Volodymyr Zelenskiy alipotembelea Ikulu ya Rais mjini Kyiv, Ukraine, kutangaza msaada mkubwa wa kijeshi wa shilingi bilioni 2.5, Januari 12, 2024.
Waziri Mkuu Rishi Sunak azungumza na Rais Volodymyr Zelenskiy alipotembelea Ikulu ya Rais mjini Kyiv, Ukraine, kutangaza msaada mkubwa wa kijeshi wa shilingi bilioni 2.5, Januari 12, 2024. © Stefan Rousseau/Pool via REUTERS
Matangazo ya kibiashara

Rishi Sunak atakutana na mwenzake wa Poland Donald Tusk, pamoja na mkuu wa NATO Jens Stoltenberg, kwa majadiliano juu ya Ukraine na, kwa upana zaidi, usalama wa Ulaya.

Ziara hii inafanyika wakati ambapo Kyiv inawasihi washirika wake kuongeza msaada wao wa kijeshi, haswa kwa kutoa risasi na vifaa vingine, muhimu kwa kuzima mashambulio ya Urusi.

Siku ya Jumamosi, baada ya mazungumzo marefu na magumu, Baraza la Wawakilishi la Marekani lilipigia kura mpango mkubwa wa msaada wa dola bilioni 61 kusaidia Kyiv.

Kabla tu ya kuondoka kuelekea Poland, Bw Sunak alizungumza na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky "kumhakikishia uungaji mkono usioyumba wa Uingereza kwa ulinzi wa Ukraine dhidi ya matarajio ya kikatili na ya kujitanua ya Urusi, kulingana na msemaji wa Downing Street."

Waziri Mkuu wa Uingereza "amethibitisha kwamba Uingereza itatoa nyongeza ya pauni milioni 500 katika ufadhili wa haraka kusaidia uwezo wa haraka zaidi, pamoja na mabomu ya ziada, ulinzi wa anga na ndege zisizo na rubani - na kuleta msaada wetu mwaka huu hadi pauni bilioni 3", kulingana na chanzo hiki.

"Wizara ya Ulinzi pia itatoa ahadi kubwa ya kihistoria ya zana za kijeshi kusaidia Ukraine kufaya mashambulizi ya nchi kavu, baharini na angani," msemaji huyo amesema.

- Tishio lililopo -

"Nilizungumza na Bw. Zelensky asubuhi ya leo (...) nikiwa ndani ya gari nikielekea uwanja wa ndege. Tulizungumza kuhusu ulinzi wa anga, mojawapo ya mada nyingi zilizojadiliwa," Bw. Sunak amewaambia waandishi wa habari kwenye ndege.

"Utaona kwamba kifurushi tulichotangaza leo ni kikubwa zaidi ya kile tumewahi kutangaza kwa siku moja," ameongeza.

Vifaa vilivyotumwa Ukraine na Wizara ya Ulinzi ni pamoja na boti 60, zaidi ya makombora 1,600, haswa kwa ulinzi waanga, pamoja na makombora ya masafa marefu ya Storm Shadow. Zaidi ya hayo ni karibu risasi milioni nne za silaha ndogo ndogo.

Bw. Zelensky alikaribisha tangazo la usafirishaji mpya.

"Makombora ya Storm Shadow na mengine, mamia ya magari ya kivita na boti, risasi, yote haya yanahitajika kwenye uwanja wa vita," amesema katika mtandao wa X.

Rais wa Ukraine ameishukuru Uingereza kwa usaidizi huu wa ulinzi ambao unazingatia uwezo wa baharini na masafa marefu.

Bw. Zelensky pia ameripoti kuwa amejadiliana na Bw. Sunak "haja ya kuwa na mtindo mzuri wa kunyang'anywa mali za Urusi zilizozuiwa" kote ulimwenguni.

"Kuilinda Ukraine dhidi ya matarajio ya kikatili ya Urusi ni muhimu kwa usalama wetu na kwa Ulaya yote," Rishi Sunak alisema katika taarifa ya asubuhi.

Ikiwa Putin atashinda "vita hivi vya uchokozi, hataishia kwenye mpaka wa Poland," alionya Waziri Mkuu wa Uingereza.

Ukraine "inakabiliwa na tishio lililopo" huku "Urusi ikiendelea na uvamizi wake wa kinyama, na kuhatarisha usalama na utulivu wa Ulaya yote," Downing Street imeandika.

Akiwa na Donald Tusk, Rishi Sunak pia atajadili "kuongezeka" kwa uhusiano wa nchi mbili.

Mkuu wa serikali ya Uingereza kisha atakutana na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz mjini Berlin.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.