Ujerumani yahalalisha bangi kwa matumizi ya burudani
Nairobi – Ujerumani imekuwa nchi kubwa ya Umoja wa Ulaya kuhalalisha bangi kwa kwa matumizi ya burudani licha ya pingamizi kali kutoka kwa wanasiasa wa upinzani na wanaharakati wa masuala ya afya wanaosema hatua hiyo itaongeza matumizi yake miongoni mwa vijana.
Imechapishwa:
Hatua hiyo ina maana kwamba watu wenye umri wa zaidi ya miaka 18 sasa wanaruhusiwa kubeba gramu 25 za bangi kavu na kulima hadi mimea mitatu ya bangi katika makaazi yao.
Aidha, hii inamaanisha kuwa bangi sio marufuku nchini Ujeremani na hii ni habari njema kwa watumiaji wanaokadiriwa kufikia Milioni 4.5.
Wizara ya afya inasema hatua hii itasaidia kuzuia masoko yasiyo rasmi yanayouzwa bangi, yanayozalisha Euro Bilioni 4 kila mwaka.
Kuanzia Julai mosi, watu wazima wataruhusiwa kununua bangi kutoka kwa vilabu vya watu wasiozidi mia tano ambao kila mmoja atapata hadi gramu hamsini za bangi kila mwezi.
Hata hivyo wanaharakati wa afya wanapinga hatua hiyo kwa msingi kuwa matumizi ya bangi miongoni mwa vijana yataathiri mfumo wa maisha kwa watumiaji.