Pata taarifa kuu

Mgogoro wa uhamiaji Lampedusa, kiini cha shughuli kubwa ya kidiplomasia

Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen atazuru kisiwa kidogo cha Italia cha Lampedusa Jumapili hii, Septemba 17, ambako maelfu ya wahamiaji waliwasili wiki hii, na kuzindua upya mjadala mzito wa kugawana majukumu ndani ya Umoja wa Ulaya.

Boti inayowabeba wahamiaji ikiwasili huko Lampedusa, Septemba 16, 2023.
Boti inayowabeba wahamiaji ikiwasili huko Lampedusa, Septemba 16, 2023. AP - Cecilia Fabiano
Matangazo ya kibiashara

Mgogoro wa uhamiaji unaoathiri Lampedusa umekuwa mada ya shughuli kubwa za kidiplomasia kwa saa 48. Ulikuwa tena katikati ya mazungumzo ya simu Jumamosi hii kati ya Emmanuel Macron na Giorgia Meloni. Rais wa Ufaransa na mkuu wa serikali ya Italia wamejitolea "kuimarisha ushirikiano katika ngazi ya Ulaya (...) ili kupata ufumbuzi wa ufanisi, wa haraka na wa muda mrefu wa mgogoro huu". Viongozi hao wawili pia wamejadili "hatua ya pamoja" ambayo inaweza kufanywa na Paris na Roma katika Bahari ya Mediterania, wimeongeza ikulu ya Élysée bila maelezo zaidi.

Mkutano wa simu pia umewaleta pamoja Jumamosi alasiri mawaziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa, Italia na Ujerumani, mwakilishi wa ofisi ya rais wa Uhispania wa Baraza la Umoja wa Ulaya na Kamishna wa Mambo ya Ndani wa EU Ylva Johansson. Mkutano huo ulipendekezwa na Waziri wa Ufaransa Gérald Darmanin, ambaye tayari alikuwa amekutana Ijumaa asubuhi na wenzake wa Italia, Matteo Piantedosi, na wa Ujerumani, Nancy Faeser. Hata hivyo, hakuna chochote kilichovuja kutoka kwa mazungumzo yao.

Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen atazuru Jumapili hii kisiwa cha Lampedusa akiambatana na kwa mwaliko wa Giorgia Meloni, ambaye siku ya Ijumaa jioni aliomba kwamba suala la uhamiaji liwekwe kwenye ajenda ya mkutano ujao wa kilele wa EU mwezi Oktoba. "Shinikizo la wahamaji ambalo Italia imekuwa ikipata tangu mwanzoni mwa mwaka si endelevu," alisema mkuu wa serikali ya Italia, ambaye anaongoza muungano wa mrengo wa kulia na wa mrengo mkali wa kulia.

Kutokana na uhaba wa nafasi katika kituo cha mapokezi cha Lampedusa, mamia ya watu wamelazimika kulala nje, barabarani, wakati mwingine wakinufaika na ukarimu wa wakazi waliowaletea maji na chakula. Jumla ya wahamiaji zaidi ya 127,000 wametua kwenye fuo za Italia tangu kuanza kwa mwaka huu, karibu mara mbili ikilinganishwa na kipindi kama hicho mnamo mwaka 2022.

(Pamoja na AFP)

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.