Pata taarifa kuu
MUUNGANO-SIASA

Tanzania yaadhimisha miaka 60 ya muungano

Tanzania inaadhimisha leo miaka 60 ya muungano wa iliyokuwa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar unaotajwa kuwa alama ya juhudi za kuliunganisha bara la Afrika baada ya kipindi cha ukoloni.

Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan wakati wa ziara yake nchini Afrika Kusini mwezi Machi, 2023.
Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan wakati wa ziara yake nchini Afrika Kusini mwezi Machi, 2023. AFP - PHILL MAGAKOE
Matangazo ya kibiashara

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulitokea tarehe 26 Aprili 1964 ukawa mwanzo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hadi tarehe ile kulikuwa na mataifa mawili huru ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambayo yaliingia mkataba wa muungano mnamo mwaka 1964 na kuanzishwa dola la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika miaka ya karibuni, wanasiasa hususan kutoka upande wa upinzani wamekuwa wakishinikiza mageuzi ya muundo wa muungano huo ulioasisiwa na kiongozi wa kwanza wa Tanganyika, Julius Nyerere na rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume

Mkataba wa Muungano

Mkataba wa Muungano ulitiwa saini na aliyekuwa Rais wa Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, tarehe 22 Aprili 1964 huko Zanzibar. Mkataba huo ulithibitishwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi tarehe 26 Aprili 1964.

Tarehe 27 Aprili 1964, viongozi wa nchi zote mbili walikutana katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam na kubadilishana Hati za Muungano.

Mabadiliko ya jina

Jina la “Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar” lilibadilishwa baadaye, tarehe 28 Oktoba 1964, na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitia Sheria ya Jamhuri ya Muungano, Sheria namba 61 ya mwaka 1964.

Sababu ya Muungano

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umekuwepo kutokana na sababu mbalimbali kama vile kuwepo kwa mahusiano ya karibu na ya kihistoria baina ya Tanganyika na Zanzibar katika nyanja mbalimbali kama vile undugu wa damu, biashara, utamaduni, lugha na mahusiano ya karibu kisiasa hususan baina ya vyama vya TANU na ASP.

Pia, azma ya kuwa na Muungano wa Afrika, hususan kwa kuanzia na Shirikisho la Afrika Mashariki. Hata kabla ya uhuru wa Tanganyika, Mwalimu Nyerere pamoja na viongozi wengine waliokuwa wakipigania uhuru katika ukanda wa Afrika walikuwa na matarajio ya kuwa na Muungano wa Afrika. Mwalimu Nyerere binafsi alipendelea uwepo Muungano wa Afrika kwa kuanzia na Mashirikisho ya kikanda.

Kimsingi zipo sababu mbalimbali zilizosababisha Muungano huu kama vile historia za nchi hizo mbili, ukaribu wa nchi hizi mbili, muingiliano wa kijamii, ushirikiano wa kibiashara, ushirikiano madhubuti na wa muda mrefu wa kisiasa baina ya TANU na ASP, ushirikiano na urafiki wa muda mrefu kati ya watu, viongozi, na wakati wa harakati za utaifa uliopelekea uhuru wa nchi hizo mbili.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.