Tahadhari yaendelea kuhusu kimbunga Hidaya nchini Kenya na Tanzania
Maeneo ya ukanda wa Pwani nchini Kenya na Tanzania, yanashuhudia upepo mkali, huku mamlaka ya utabiri wa hali ya hewa, zikitoa tahadhari ya uwekezekano wa kutokea kwa kimbunga Hidaya, kitakachoambatana na mvua kubwa.
Imechapishwa:
Nchini Tanzania, usafiri wa boti na vivuko kati ya Dar es salaam na Zanzibar zimesitishwa hadi siku ya Jumatatu, baada ya kutolewa kwa tahadhari ya maeneo ya Pwani kukumbwa na kimbunga hidaya.
Wakaazi maeneo hayo waliozungumza na RFI Kiswahili wamesema kuanzia jana walianza kushuhudi upepo mkali, huku kisiwa cha Mafia kikiathrika.
"Upepo mkali umekuwepo toka jana usiku," Steven Mumbi, mwandishi wetu wa Dar es salaam amesema.
MWENENDO WA KIMBUNGA “HIDAYA” KATIKA BAHARI YA HINDI MASHARIKI MWA PWANI YA TANZANIA.
— Tanzania Meteorological Authority (@tma_services) May 4, 2024
Saa 05:00 Asubuhi ya leo tarehe 04 Mei 2024.
Kwa taarifa zaidi tembelea: https://t.co/K0zVP2RUDM #KimbungaHidaya#CycloneHidaya pic.twitter.com/LZFBVmuK98
Wataalam wanaonya kuwa kimbunga hicho kinatarajiwa kuwa kikubwa, katika siku zijazo.
Mamlaka ya utabiri wa hali ya hewa nchini Kenya siku ya Jumamosi imesema athari za kimbunga hidaya zimeanza kushuhudiwa kutokana na upepo mkali unaoendelea kuvuma, hali inayotarajiwa kuendelea kwa siku mbili zijazo.
🌊 Taarifa ya hali ya hewa baharini karibu na mwambaa wa Kenya imechapishwa! Imetolewa saa 15:00 EAT tarehe 4 Mei, 2024, na ni halali kutoka saa 00:00 EAT tarehe 5 Mei, 2024 hadi saa 00:00 EAT tarehe 6 Mei, 2024. Kaa tayari kwa maelezo zaidi! #HaliYaHewaBaharini #Kenya 🇰🇪 pic.twitter.com/SLQNhulfoE
— Kenya Met Department 🇰🇪 (@MeteoKenya) May 4, 2024
Wakaazi wa maeneo ya Pwani ya nchi hizo mbili na Kusini mwa Tanzania, wametakiwa, kuendelea kuchukua tahadhari.
Tahadhari ya kimbunga hiki inakuja, wakati huu Kenya na Tanzania zikiendelea kushuhudia mvua kubwa iliyosababisha mafuriko, yaliyoleta maafa ya zaidi ya watu 400 na maelfu kulazimika kuyahama makaazi yao baada ya kusombwa na maji.