Pata taarifa kuu
UFARANSA-SIASA

Rais Macron amteua Edouard Phillippe kuwa Waziri Mkuu

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amemteua Edouard Philippe mwenye umri wa miaka 46 kuwa Waziri Mkuu mpya.

Waziri Mkuu wa Ufaransa Edouard Phillippe
Waziri Mkuu wa Ufaransa Edouard Phillippe CHARLY TRIBALLEAU / AFP
Matangazo ya kibiashara

Philippe ambaye hafahamiki sana kisiasa nchini humo ametokea katika chama cha Republican ambacho wachambuzi wa siasa wanaona kuwa sera zake zinaendana ana sera za vuguvugu la République En Marche la rais Macron.

Akizungumzia uteuzi huu, mwanasiasa Jean-Luc Mélenchon aliyewania urais na kumaliza wa tatu katika mzunguko kwa kwanza, amesema uamuzi wa kumteua mwanasiasa huyu kutoka chama cha Republican ni ishara kuwa mabadiliko makubwa yasitarajiwe katika serikali yake.

Philippe licha ya kuwa mwanasiasa, pia ni wakili na amekuwa mbunge wa eneo la Seine-Maritime tangu mwaka 2012.

Awali, alihudumu pia kama Meya wa mji wa Le Havre Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyo kati ya mwaka 1995 hadi 2010.

Atakumbukwa pia kuongoza kampeni za rais wa zamani Jacques Chirac mwaka 2002, na kusaidia kuchaguliwa kwake.

Mwaka 2007, alihudumu katika kama Waziri wa Mazingira baada ya kuteuliwa na Waziri Mkuu wa wakati huo Allain Juppe, wadhifa ambao alihudumu kwa muda mfupi.

Wachambuzi wa siasa nchini Ufaransa wanasema ni muhimu kwa rais Macron kufanya uteuzi kama huu ikiwa anataka kushinda idadi kubwa ya viti bungeni mwezi ujao.

Wiki iliyopita, Philippe ambaye hakufahamu kama atateuliwa katika wadhifa huu alitoa wito kwa Macron kufanya uteuzi kutoka pande zote za kisiasa kama njiamojapo ya kuliunganisha kwa haraka taifa hilo ambalo limegawanyika kisiasa.

Huu ndio uteuzi mkubwa na wa kwanza, kufanya na rais mpya wa Ufaransa Emmanuel Macron aliyeapishwa Jumapili iliyopita.

Orodha ya Mawaziri Wakuu miaka ya hivi karibuni:-

  • Dominique de Villepin-2005 -2007
  • François Fillon-2007- 2010
  • Jean-Marc Ayrault-2012-2012
  • Manuel Valls-2014-2016
  • Bernard Cazeneuve -2016-2017
  • Edouard Philippe-2017-Waziri Mkuu wa sasa
Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.