Pata taarifa kuu
TANZANIA

Magufuli achaguliwa kwa kishindo kuwa mwenyekiti mpya wa CCM

Wajumbe wa mkutano mkuu wa chama tawala nchini Tanzania, CCM, kwa pamoja wamepiga kura ya ndiyo, kumuidhinisha rasmi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli, kuwa mwenyekiti wa tano wa chama hicho.

Mwenyekiti mpya wa chama tawala nchini Tanzania, CCM na Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli.
Mwenyekiti mpya wa chama tawala nchini Tanzania, CCM na Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli. DR
Matangazo ya kibiashara

Wajumbe walioshiriki kwenye mkutno mkuu na kupiga kura, walikuwa ni 2398, ambapo mara baada ya zoezi la upigaji kura, mwenyekiti anayemaliza muda wake, Jakaya Kikwete, alimtangaza Rais Magufuli kama mshindi kwa kupata kura zote za ndiyo.

Awali kwenye kuelekea mkutano huu maalumu wa CCM, kulikuwa na taarifa za uwepo wa mgawanyiko ndani ya chama, na taarifa kuwa mwenyekiti anayemaliza muda wake alikuwa hataki kuachia nafasi hiyo, tuhuma ambazo zilikanushwa na Kikwete na Rais Magufuli.

Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi na kukabidhiwa rasmi vitendea kazi kama mwenyekiti wa chama, Rais Magufuli, aliwashukuru wajumbe wa mkutano mkuu, kwa kuendelea kumuunga mkono toka aliposhinda kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Rais Magufuli amesema kuwa, awali wakati rais Kikwete akimgusia kuhusu kumkabidhi nafasi ya uenyekiti wa chama, alikataa, hali iliyosababisha wazee wa chama kuingilia kati na hatimaye kumshawishi kukubali.

Kwenye hotuba yake, Rais Magufuli amesisitiza umuhimu wa umoja wa mshikamano ndani ya chama, kama nguzo muhimu ya kufikia malengo na utekelezaji wa ilani ya chama chao.

Mwenyekiti huyo mpya, ameapa kupambana na ufisadi kama njia ya kuhakikisha anakomesha vitendo vya rushwa ndani ya chama na kwenye taifa kwa ujumla.

Miongoni mwa masuala ambayo Rais Magufulu amesema ataanza nayo pindi atakapoanza kazi ni pamoja na :

Utendaji kazi wa chama, mfumo wa uongozi, kuondoa na kupunguza baadhi ya vyeo ambavyo havina msingi ndani ya chama, maslahi ya wafanyakazi wa chama tawala, kupitia na kuhakiki mali za chama, umoja na mshikamano, mapambano dhidi ya Rushwa pamoja na kuhakikisha chama kinaongeza idadi kubwa ya wanachama.

Rais Magufuli amesema pia, atahakikisha anawaondoa wasaliti wa ndani ya chama na kwamba katika utawala wake hatakubali kuwa na wanachama ambao ni wasaliti.

Magufuli ameongeza kuwa wakati wa uongozi wake, atahakikisha chama kinajitegemea kwa rasilimali badala ya kuwa omba omba kwa wafadhili ili kiendeshe shughuli zake.

Utekelezaji wa asilimia mia moja wa ilani ya chama chake, ni miongoni mwa masuala ambayo Rais Magufuli amesema atahakikisha anafanikisha.

Magufuli anakuwa mwenyekiti wa tano wa chama tawala nchini Tanzania, baada ya watangulizi wake, aliyekuwa muasisi wa chama hicho, marehemu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete ambao wote hawa walikuwa marais wa Tanzania kwa nyakati tofauti.

 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.