Pata taarifa kuu
TANZANIA

Magufuli awaambia wapinzani kuacha siasa na kufanya kazi

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amewataka wanasiasa wa upinzani nchini humo kuacha siasa kila wakati na kuwatumikia wananchi wa taifa hilo.

Rais John Magufuli
Rais John Magufuli AFP Photo/Daniel Hayduk
Matangazo ya kibiashara

Kauli ya Magufuli inakuja wakati huu wanasiasa wa upinzani wakisusia vikao vya bunge kwa madai kuwa wanabaguliwa na naibu Spika Ackson Tulia lakini pia kuzuiliwa na polisi kufanya mikutano ya kisiasa.

Kiogozi huyo aliyeingia madarakani mwaka uliopita, amekuwa akishtumiwa na upinzani kwa kuminya uhuru wa kujieleza na kurudisha nyuma juhudi zilizopigwa kidemokrasia.

Hivi karibuni, kiongozi wa chama cha upinzani CHADEMA Freeman Mbowe, alikamatwa na polisi mjini Mwanza huku mkutano wa mbunge mwingine wa upinzani Zitto Kabwe ukivunjwa na polisi kwa kile walichokisema ni kwa sababu za kiusalama.

Akizungumza katika Ikulu ya Dar es salaam baada ya kupokea ripoti ya Uchaguzi Mkuu uliopita, rais Magufuli amesema yuko tayari kushirikiana na wanasiasa hao ili kufanikisha maendeleo ya nchi yao.

Kuhusu uchaguzi Mkuu uliopita, Tanzania bara na Visiwani Zanzibar, amesema uchaguzi huo ulikuwa huru, haki na wazi na kuahidi kuwa hivi karibuni, nchi hiyo itaingia kwenye mchakato wa kufanikisha upatikanaji wa katiba mpya.

Hata hivyo, upinzani ukiongozwa na aliyekuwa mgombea wake Edward Lowassa, ulikataa kutambua matokeo ya uchaguzi Mkuu na kudai kulitokea wizi wa kura.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.