Ukraine yatia saini mkataba wa Kihistoria na Umoja wa Ulaya
Ukraine imetia saini mkataba wa ushirikiano wa kibiashara na kisiasa na Umoja wa Ulaya jijini Brussels nchini Ubelgiji baada ya mvutano wa muda mrefu kati ya serikali iliyopita na waandamanaji na kusabibisha machafuko nchini humo.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Rais wa Ukraine Petro Poroshenko amesema hatua ya nchi yake kutia saini mkataba huo siku ya Ijumaa ni ya Kihistoria na inalenga kuinua uchumi wa nchi hiyo pamoja na kuimarisha uhusiano wake na EU katika siku zijazo.
“Mkataba huu utaimarisha uhusiano wetu wa kibiashara na kisiasa na Umoja wa Ulaya, na kutoa mtazamo mpya wa nchi yangu,” Poroshenko amesema akiwa Brussels.
“ Ni siku ya Kihistoria, siku muhimu sana tangu Uhuru wetu kutoka kwa Urusi mwaka 1991,” aliongezea.
Mbali na Ukraine, Umoja wa Ulaya unatishia mkataba wa ushirikiano na nchi za Georgia na Moldova ambayo ni ishara tosha kuwa mataifa hayo yameamua kushirikiana na mataifa ya Magharibi badala ya Urusi.
Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Herman Van Rompuy ameyahakikishia mataifa hayo kuwa " Umoja wa Ulaya hautawaacha tutashirikiana nanyi katika maswala mengi na hii ni siku kubwa kwa Umoja wa Ulaya.,"
Mwaka uliopita, hatua ya rais wa zamani wa Ukraine, Viktor Yanukovych kukataa kutia saini mkataba huo na EU ulisababisha maandamano na machafuko nchini humo na kusabisha rais huyo kukimbilia nchini Urusi.
Kipindi hiki chote Urusi imekuwa ikipinga hatua ya Ukraine kushirikiana na Umoja wa Ulaya badala ya kuegemea upande wao.
Wakati uo huo, viongozi wa Umoja wa Ulaya wameipa Urusi siku tatu kubadilisha sera yake kuhusu Ukraine la sivyo itaiwekea vikwazo zaidi.
Viongozi hao wameitaka Moscow kuja na mbinu kufikia Jumatatu ijayo kumaliza kwa amani la sivyo watachukua hatua zaidi.
Rais wa Urusi Vladimir Putin, amesema hatua ya Ukraine kuingia katika mkataba huo na Umoja wa Ulaya itasababisha nchi hiyo kugawanyika mara mbili.
Umoja wa Mataifa nao unasema watu waliokimbia makwao kutokana na machafuko Mashariki mwa nchi hiyo ni zaidi ya 110,000 wengi wameondoka nchini humo.