Pata taarifa kuu
KENYA-MIGUNA-NASA

Kenya: Idara ya uhamiaji yamtaka Miguna kuomba tena uraia wake

Idara ya uhamiaji nchini Kenya imesema imemtumia fomu mwanasheria na mwanaharakati wa vuguvugu la NRM nchini Kenya Miguna Miguna ili azijaze kuomba tena uraia wa Kenya na kumuwezesha kuingia tena nchini humo.

Mwanaharakati wa Nasa na vuguvugu la NRM nchini Kenya, Miguna Miguna.
Mwanaharakati wa Nasa na vuguvugu la NRM nchini Kenya, Miguna Miguna. Screenshot CitzenTV
Matangazo ya kibiashara

Miguna ambaye alipambana na kuishinda Serikali katika jaribio lao la kutaka kumrejesha tena nchini Canada kupitia Dubai usiku wa kuamkia leo ambapo mwenyewe amesisitiza kuwa ni raia wa Kenya na haitaji kusalimisha nyaraka zake za kusafiri ili zipigwe muhuri.

Hata hivyo kaimu mkurugenzi wa idara ya uhamiaji nchini Kenya Joseph Munywoki amesisitiza kuwa mwanaharakati huyo alipoteza haki ya kuwa raia wa nchi hiyo mwaka 1998 wakati alipokuwa rasmi raia wa Canada na wakati huo nchi ya Kenya ilikuwa hairuhusu uraia wa nchi mbili.

Baada ya Miguna Miguna kuleta taharuki kwenye uwanaja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta na hata kuvutana mashati na maofisa wa idara ya uhamiaji na kugoma kuingia kwenye ndege aliyotaiwa kusafiri nayo kwenda Dubai, idara ya uhamiaji iliamua kumuachia na kumpa fomu hizo.

“Ili kuruhusu Miguna kupata tena uraia wake, idara ya uhamiaji imemtumia fo,mu maalumu azijaze kuomba tena kwa utaratibu,” imesema taarifa ya uhamiaji.

Munywoki ambaye anakaimu ukurugenzi wa idara ya uhamiaji, amesema ili Miguna aruhusiwe kuingia nchini humo kama raia wa Kenya ni lazima ajaze fomu hizo upya kuomba kuwa raia wa Kenya.

Mkurugenzi huyo amesema hata hivyo mpaka sasa mwanaharakati huyo wa NASA hajajaza fomu hizo.

Ameongeza kuwa Miguna aligoma kutoa nyaraka zake za kusafiria kwaajili ya ukaguzi na kupigwa muhuru kama sheria inavyotaka pamoja na zile sheria za kimataifa.

Mwanasheria huyo aliwasili nchini Kenya akitokea Canada maajira ya 2.30 kwa saa za Afrika Mashariki akiwa amepanda ndege ya shirika la Emirates.

Wizara ya mambo ya ndani imesema kuwa katika kutekeleza maagizo ya mahakama walimuomba miguna awasilishe nyaraka zake alizotumia kusafiria ili aruhusiwe kuingia nchini humo lakini hakufanya hivyo.

Idara ya uhamiaji nchini Kenya mwezi mmoja uliopita ilimfurusha nchini humo Miguna kwa kile ilichodai anatishia usalama wa taifa na kwamba sio raia wa Kenya baada ya kuukana.

Tangu kumalizika kwa uchaguzi wa marudio mwezi Octoba mwaka jana, Miguna amekuwa akiongoza harakati za vuguvugu la Nasa akipinga ushindi wa rais Uhuru Kenyatta ambapo amekuwa mkosoaji mkubwa wa Serikali na hata kutishia kuchoma picha za rais.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.