Pata taarifa kuu
TANZANIA-UFARANSA

Ufaransa: Tuna imani Tanzania na Uganda zitasaini mkataba wa EPA

Nchi ya Ufaransa imesema inaamini Serikali ya Uganda na Tanzania zitatia saini mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi na umoja wa Ulaya maarufu kama EPA.

Mkurugenzi wa Africa na ukanda wa nchi za bahari ya Hindi, Remi Marechaux akifanya mahojiano na mtangazaji wa rfikiswahilim Emmanuel Makundi. 4 Machi, 2017
Mkurugenzi wa Africa na ukanda wa nchi za bahari ya Hindi, Remi Marechaux akifanya mahojiano na mtangazaji wa rfikiswahilim Emmanuel Makundi. 4 Machi, 2017 RFI Kiswahili
Matangazo ya kibiashara

Akizungumza kwenye mahojiano maalumu na idhaa hii mkurugenzi wa Afrika kutoka wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa, Remi Marechaux, amesema mkataba huu utakuwa na manufaa kwa Tanzania hadi pale itakapofikia kiwango cha nchi ya kipato cha kati.

Marechaux amesema mkataba huu hauna lengo baya kwa Tanzania wala Afrika Mashariki kama baadhi ya wachambuzi wanavyodai, badala yake inafaa wautazame kwa jicho la pili.

Marechaux amesema "Hii ni changamoto lakini tunaamini kuwa Uganda na Tanzania zote kwa pamoja zitatia saini mkataba huu wa ushirikiano wa kiuchumi na umoja wa Ulaya, kwa sababu hata hivyo haiitaji sana kutia saini kwakuwa tayari inanufaika kwa vitu vingi. Lakini kwa kuzingatia kuwa Tanzania inaelekea kwenye uchumik wa kati..pale itakapofikia hapo haitakuwa na haja tena ya kunufaika kwenye mkataba huu kwa hivyo ni lazima ijiandae kwa mabadiliko haya".

Kuhusu hofu iliyokuwepo kwa wawekezaji kutoka Ufaransa kuja kuwekeza nchini Tanzania, Marechaux amesema baada ya kupata hakikisho kutoka kwa Serikali kuhusu kuboreshwa kwa mazingira ya uwekezaji, anaamini makampuni zaidi ya Ufaransa yatakuja Tanzania.

Nembo inayotumika kwenye mkutano wa jukwaa la kibiashara kati ya Ufaransa na Tanzania
Nembo inayotumika kwenye mkutano wa jukwaa la kibiashara kati ya Ufaransa na Tanzania Emmanuel Makundi/RFIKIswahili

Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa ili wawekezaji wavutiwe ni lazima nchi za ukanda ziwe na usalama wa kutosha, ambapo akatumia fursa hii kupongeza juhudi ambazo zimechukuliwa na Serikali ya Kenya katika kudhibiti vitendo vya kigaidi hasa baada ya mashambulizi ya Wetsgate na Garrisa.

Kuhusu hali ya Burundi, Marechaux amesema nchi yake inapongeza juhudi ambazo zimeendelea kufanywa na mratibu wa mazungumzo ya amani ya Burundi, rais mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa, ambapo amesema licha ya changamoto kutoka kwa makundi yanayoshiriki mazungumzo hayo, wanavutiwa na juhudi zinazoendelea kufanywa.

"Licha ya kuwa kwenye mkutano uliipita wa Arusha baadhi ya wanasiasa walisusia, Ufaransa bado inaamini hata hivyo kufanyika tu kwa mkutano ni ishara tosha ya kupiga hatua." alisema Marechaux.

Kuhusu Sudan Kusini, Marechaux amesema hali inayoendelea kushuhudiwa nchini humo inasikitisha na hasa wakati huu kukiwa na janga la kibinadamu na njaa.

Amesema nchi ya Ufaransa inaendelea kushirikiana na nchi washirika za ukanda na jumuiya za ukanda kama IGAD, EAC na Umoja wa Afrika katika kuhakikisha wanapata suluhu ya kudumu kuhusu mzozo wa Sudan Kusini.

"Ufaransa imeendelea kushirikiana na Jumuiya za ukanda kuhakikisha suluhu inapatikana, licha ya kuwa ukweli ni kwamba tunaguswa sana na hali mbaya ya kibinadamu tunayoishuhudia nchini humo." aliongeza Marechaux.

Haya ameyasema kando na kongamano la kibiashara kati ya Tanzania na Ufaransa ambalo limeng’oa nanga hapo jana na linahudhuriwa na wawakilishi wa Serikali zote mbili.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.