Pata taarifa kuu

Haiti: Watu 19,000 wamefikia kiwango cha juu zaidi cha uhaba wa chakula

Haiti inakabiliwa na janga la kibinadamu huku takriban watu 19,000 huko Cité-Soleil, mojawapo ya vitongoji duni vikubwa zaidi vya Port-au-Prince, wakiwa wamefikia kiwango cha juu cha uhaba wa chakula, shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa, WFP, limeonya, Ijumaa tarehe 14 Oktoba.

Cité-Soleil, mojawapo ya vitongoji duni vikubwa zaidi vya Port-au-Prince.
Cité-Soleil, mojawapo ya vitongoji duni vikubwa zaidi vya Port-au-Prince. © Ricardo Arduengo / REUTERS
Matangazo ya kibiashara

"Watu 19,000 huko Cité-Soleil wanakabiliwa na maafa kwa sababu hawana chakula cha kutosha [...]. Hiyo ina maana pengine wana mlo mmoja tu kwa siku, na hakuna protini, mboga mboga, au kirutubisho kingine chochote muhimu ambacho watu wanahitaji ili kuishi," Mkurugenzi wa WFP nchini Haiti, Jean-Martin Bauer amewaambia waandishi wa habari kwa njia ya video.

"Ni mara ya kwanza nchini Haiti" kunaripotiwa watu walioainishwa katika awamu ya tano, ya juu zaidi ya uainishaji wa usalama wa chakula (CIP), amebainisha. Haiti, nchi inayohangaika na msukosuko wa kisiasa wa miaka mingi, ambayo inakumbwa na magenge ya wahalifu, sasa pia imekumbwa na kipindupindu.

Maafa ya kibinadamu nchini Haiti

Nchi hii pia inakabiliwa na mfumuko mkubwa wa bei. Na tangu Haiti itangaze kupanda kwa bei ya gesi mwezi Septemba, nchi hiyo imeshuhudia ghasia, visa vya uporaji na maandamano dhidi ya Waziri Mkuu Ariel Henry. 

Tarehe 9 Oktoba Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kutuma wanajeshi wake kuisaidia Haiti ambayo imetoa wito wa kusaidiwa kupambana na magenge ya uhalifu. 

Hivi karibuni maelfu ya raia wa Haiti walifanya maandamano huko Port-au-Prince kupinga serikali na wito wake wa msaada kutoka nje ili kukabiliana na ukosefu wa usalama, mzozo wa kibinadamu na janga la kipindupindu.

"Haiti inakabiliwa na maafa ya kibinadamu [...] na ripoti iliyotolewa leo inaonyesha kwamba ukubwa na kiwango cha uhaba wa chakula nchini Haiti kinazidi kuwa mbaya," amesema Jean-Martin Bauer. Ripoti hiyo inaonyesha kuwa watu milioni 4.7 nchini Haiti wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, ambapo "milioni 1.8 wanakabiliwa na viwango vya dharura vya uhaba wa chakula", amebainisha afisa huyo wa WFP. Idadi hii imeongezeka katika kipindi cha miezi sita iliyopita.

"Tumeona ongezeko la watu 200,000 wakikabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na ongezeko la watu nusu milioni wakikabiliwa na uhaba wa chakula wa dharura," kina Jean-Martin Bauer.

(pamoja na AFP)

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.