Pata taarifa kuu
USALAMA-JAMII

Makumi ya watu watekwa nyara kaskazini magharibi mwa Nigeria

Watu wenye silaha waliwateka nyara makumi ya watu katika jimbo la kaskazini-magharibi mwa Nigeria la Kaduna siku ya Jumanne, siku chache baada ya kutekwa nyara kwa zaidi ya wanafunzi 250 wa shule moja katika jimbo hilo, maafisa wawili wa eneo hilo na chanzo cha Umoja wa Mataifa wamesema.

Magenge ya wahalifu mara kwa mara huteka nyara watu wengi kaskazini-magharibi mwa Nigeria.
Magenge ya wahalifu mara kwa mara huteka nyara watu wengi kaskazini-magharibi mwa Nigeria. © AFP
Matangazo ya kibiashara

Kulingana na diwani wa eneo hilo Abubakar Buda aliyehojiwa na kituo cha televisheni cha Channels TV nchini Nigeria, watu wenye silaha walivamia kijiji kimoja wilayani Kajuru siku ya Jumanne asubuhi na kwenda nyumba kwa nyumba wakiwateka nyara wakaazi, na kufyatua risasi mara kwa mara. Uingiliaji kati wa kijeshi uliweza kuzuia watu zaidi wasitekwi nyara, kulingana na kituo hicho. Wanawake 32 na wanaume 29 walitekwa nyara, mbunge wa eneo hilo Usman Danlami Stingo ameviambia vyombo vya habari vya Arise News.

Chanzo cha Umoja wa Mataifa, ambacho hakijaidhinishwa kuzungumza na waandishi wa habari, kimelithibitishia shirka la habari la AFP kwamba watu wenye silaha walishambulia kijiji hicho mapema siku ya Jumanne. "Ripoti ya awali ilionyesha watu 40 walitekwa nyara lakini idadi iliongezeka hadi karibu 60," kimesema chanzo hiki.

Utekaji nyara huu ulitokea wakati ambapo vikosi vya usalama vinawasaka zaidi ya wanafunzi 250 waliotekwa nyara mnamo Machi 7  katika shule moja, iliyoko Kuriga, katika jimbo hilo, takriban kilomita 150 kutoka kijiji hiki. Kulingana na familia za mateka hao, hawajapata taarifa yoyote tangu utekaji nyara huo wa watu wengi, mojawapo ya matukio makubwa zaidi nchini humo katika kipindi cha miaka mitatu.

Magenge ya wahalifu mara kwa mara huteka nyara watu wengi kaskazini-magharibi mwa Nigeria. Wanalenga shule, vijiji na barabara kuu, mahali ambapo wanaweza kuteka nyara watu wengi haraka, kwa lengo la kupata malipo ya fidia.

Wimbi la matukio ya utekaji nyara unaoiathiri Nigeria ni changamoto kwa serikali ya Rais Bola Ahmed Tinubu ambaye aliahidi kukabiliana na tatizo la ukosefu wa usalama, lakini pia kupambana na tatizo la gharama za maisha na kuvutia uwekezaji zaidi katika nchi hiyo yenye watu wengi zaidi barani Afrika.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.