Pata taarifa kuu
UTURUKI-UN

Uturuki yamkashifu vikali mkuu wa tume ya haki za binadamu ya UN

Nchi ya Uturuki Jumanne ya wiki hii imekashifu vikali ripoti ya umoja wa Mataifa iliyosema ni ya “upendeleo” na “haikubaliki”, ripoti ambayo imesema nchi hiyo imetekeleza vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu wakati ilipotangaza hali ya dharula.

Zeid Ra'ad al-Hussein, mkuu wa tume ya haki za binadamu ya umoja wa Mataifa. March 9, 2018.
Zeid Ra'ad al-Hussein, mkuu wa tume ya haki za binadamu ya umoja wa Mataifa. March 9, 2018. ©REUTERS/Denis Balibouse
Matangazo ya kibiashara

Katika majibu yake ya hasira kuhusu ripoti hiyo, waziri wa mambo ya nje wa Uturuki amemtuhumu mkuu wa tume ya haki za binadamu ya umoja wa Mataifa kwa kuigeuza tume hiyo kuwa mshirika wa karibu wa makundi ya kigaidi.

Uturuki inasema ripoti hiyo imejaa upotoshaji, ubaguzi na taarifa zisizo za kweli, haikubaliki kwa Uturuki, kauli inayotolewa ikiwa ni saa chache tu zimepita tangu tume ya haki za binadamu ichapishe ripoti iliyoanisha matukio yote ya mwaka 2017.

Nchi ya Uturuki imekuwa kwenye hali ya hatari tangu mwezi Julai mwaka 2016 baada ya kushinidikana kwa jaribio la mapinduzi, na makataa ya muda huo kuongezwa kwa mara ya sita mwezi Januari mwaka huu.

Ripoti ya umoja wa Mataifa inasema mamlaka makubwa yaliyotolewa kwa vyombo vya usalama imesababisha kuendelea kukiukwa kwa sheria za nchi na kuongezeka kwa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu.

Mkuu wa tume hiyo Zeid Ra’ad Al Hussein ameeleza matokeo ya uchunguzi wao kama yanaogofya, yanakasirisha na kwamba idadi ya vitendo vya ukiukaji wa binadamu inatisha.

Amesema jumla ya watu laki moja na elfu 60 wamezuiliwa katika kipindi cha miezi 18 ya hali ya hatari wakati wafanyakazi wa uma laki moja na elfu 52 wamefukuzwa kazi.

Hata hivyo Uturuki inamtuhumu Al Hussein mwenye asili ya Jordan kuwa mshirika wa karibu wa makundi ya kigaidi na kwamba ametengeneza takwimu kuichafua nchi yake.

Uturuki imeongeza kuwa Hussein “kwa bahati mbaya ameibadilisha tume hiyo kuwa chini ya uongozi ambao unashirikiana na makundi ya kigaidi”.

“Mkuu wa tume ya haki za binadamu...ameandaa ripoti hii kwa kushirikiana na makundi ya kigaidi,” imesema ripoti ya wizara ya mambo ya nje.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.