Pata taarifa kuu
DRC-UFARANSA-SIASA

Ufaransa yamtaka Kabila kuheshimu Katiba

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Marc Ayrault, kwenye runinga ya TV5 Monde Jumatatu wiki hii alizungumzia masuala mengi kuhusu hasa Syria, Libya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Wafuasi wa upinzani wakati wa maandamano mjini Kinshasa, Septemba 19, 2016.
Wafuasi wa upinzani wakati wa maandamano mjini Kinshasa, Septemba 19, 2016. AFP/EDUARDO SOTERAS
Matangazo ya kibiashara

Kuhusu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambako kulishuhudiwa hivi karibuni machafuko wakati wa maandamano ya upinzani yaliyozimwa na polisi baada ya kutumia nguvu za kupita kiasi na kusababisha vifo vya watu kadhaa Septemba 19 na 20, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa amemtaka Rais Joseph Kabila kuheshimu Katiba na kutowania katika uchaguzi wa urais.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa amesema ana hofu ya kutokea vurugu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo endapo Rais Joseph Kabila atatangaza nia yake ya kuwania katika uchaguzi wa urais. Ameomba tarehe ya uchaguzi itangazwe haraka iwezekanavyo. Amesema Ufaransa haingilii masuala ya ndani ya nchi hiyo bali nchi yake inahofia kutokea kwa machafuko nchini humo.

Bwana Ayrault amesema haungi mkono rais yeyote kung'ang'ania madaraka na kuharakia kurekebisha baadhi ya Ibara za katiba kwa minajili ya kusalia madarakani.

Hofu ya kutokea vurugu inaendelea kutanda nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baada ya pendekezo la Tume huru ya Uchaguzi (CENI).

Tume ya uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo, CENI, mwishoni mwa juma lililopita, ilisema inapanga kuomba kusogezwa mbele kwa tarehe ya uchaguzi mkuu wa rais na wabunge, uliokuwa umepangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu, sasa ufanyike mwenzi November mwaka 2018.

Tangazo la tume ya uchaguzi nchini DRC, limekuja wakati huu upinzani nchini humo ukihofia kuwa huenda rais Joseph Kabila akasalia madarakani wakati muda wake utakua umemalizika ifikapo mwezi Desemba.

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi nchini humo, Corneile Naanga, amesema kuwa wameomba uchaguzi huo usogezwe mbele ili kutoa nafasi ya kufanyika kwa maandalizi mazuri zaidi yatakayopelekea kuwa na uchaguzi ulio huru na haki.

Hata hivyo upinzani tayari umepinga pendekezo hili la tume ya uchaguzi, ambapo kwa wiki kadhaa muungano wa vyama vya siasa nchini humo unaoongozwa na mwanasiasa mkongwe Etienne Tshisekedi wa Mulumba umekuwa ukishinikiza uchaguzi kufanyika mwaka huu na rais Kabila kuondoka madarakani kwa mujibu wa Katiba.

Tangazo hili linatolewa pia, wakati huu mazungumzo ya kitaifa kusaka suluhu ya kisiasa nchini humo yakiendelea kusuasua, huku ikiwa haijulikani ikiwa kutapatikana suluhu, na hasa baada ya tangazo hili la CENI.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.