Pata taarifa kuu

Iraq: Maswali mengi baada ya 'mlipuko' mbaya kwenye kambi ya jeshi

Katikati mwa Iraq, mlipuko mkubwa uliharibu sehemu ya kambi ya wanajeshi wa Iraq karibu na Iran usiku wa Ijumaa Aprili 19 kuamkia Jumamosi Aprili 20. Katika mazingira ya mvutano huo unaosumbua kanda hii, wengi wanajiuliza kuhusu chanzo cha tukio hilo lililosababisha kifo cha mtu mmoja na majeruhi wanane.

Picha iliyochukuliwa kutoka kwenye video ya UGC iliyorushwa Aprili 20, 2024 ikionyesha moto na moshi ukipanda katika mkoa wa kati wa Babile baada ya shambulio la anga ambalo liliripotiwa kulenga usiku kambi ya kijeshi ya Iraq inayohifadhi muungano wa makundi yenye silaha yanayounga mkono Iran.
Picha iliyochukuliwa kutoka kwenye video ya UGC iliyorushwa Aprili 20, 2024 ikionyesha moto na moshi ukipanda katika mkoa wa kati wa Babile baada ya shambulio la anga ambalo liliripotiwa kulenga usiku kambi ya kijeshi ya Iraq inayohifadhi muungano wa makundi yenye silaha yanayounga mkono Iran. AFP - -
Matangazo ya kibiashara

Jumamosi hii asubuhi, kumeonekana katika kambi hiyo ya jeshi shimo lenye kina cha mita 5 na upana wa mita 10 , anaripoti mwandishi wetu huko Erbil, Iraq, Marie-Charlotte Roupie. Na hadi sasa hakuna maelezo. Kalsu ni kambi ya kijeshi katika mkoa wa Babeli, kusini mwa Baghdad. Kuna makao makuu ya kijeshi na Vikosi vya Kuhamasisha raia, Hashd al-Chaabi, makundi ya zamani ya wanamgambo yenye husiano wa karibu na Iran, leo ni sehemu muhimu ya jeshi la taifa.

Je, kambi hiyo imelengwa na ndege isiyo na rubani au makombora? Imepigwa na nani? Haraka baada ya mlipuko huo, uhusiano ulifanywa kati yake na mvutano kati ya Iran na Israeli. Na jeshi la Marekani tayari lililenga eneo hili miezi michache iliyopita, kulipiza kisasi mashambulizi dhidi ya kambi zake yaliyofanywa na makundi yenye silaha ya Iraq. Lakini wakati huu, Marekani inakanusha uhusiano wowote na shambulio lolote. Likihojiwa na shirika la hbari la AFP, jeshi la Israel kwa upande wake limebaini kwamba"halitatotoa maoni yoyote kuhusu habari zilizochapishwa katika vyombo vya habari vya kigeni".

Akizungumza na shirika la habari la AFP kwa sharti la kutotajwa jina, afisa katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iraq amehakikisha kwamba hambulio hilo lilikuwa limelenga Kurugenzi ya Magari ya Kivita ya Hachd al-Shaabi. Hachd al-Chaabi inaleta pamoja makundi kadhaa yenye silaha yanayoiunga mkono Iran, ambayo kulingana na baadhi ya vyanzo, pia yamefanya mashambulizi kadhaa nchini Iraq na Syria dhidi ya wanajeshi wa Marekani waliowekwa kama sehemu ya muungano wa kimataifa wa kupambana na wanajihadi.

"Tutalipiza kisasi dhidi ya yeyote aliye nyuma ya uchokozi huu," ameonya Abou Alaa al-Walaï, katibu mkuu wa Brigedi za Sayyed al-Shuhada, mojawapo ya makundi ambayo ni sehemu ya Hachd. "Wale wanaohusika katika uhalifu huu wa kutisha watalipa gharama," amesisitiza katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyochapishwa kwenye akaunti yake ya X.

Katika taarifa, vikosi vya usalama vya Iraq vimesema siku ya Jumamosi kwamba hakuna shughuli za angani zilizorekodiwa juu ya kambi wakati wa mlipuko huo. Je, basi inaweza kuwa ajali? Uchunguzi umefunguliwa ili kujaribu kujibu maswali haya yote.

Tukio hili la usalama nchini Iraq linakuja wakati ambapo juhudi za kidiplomasia zinaendelea kuepusha uhasama katika Mashariki ya Kati, katikati ya hali ya vita huko Gaza na kuibuka tena kwa mvutano kati ya Israel na Iran. Kabla ya mapambazuko siku ya Ijumaa, mashambulizi ya ndege zisizo na rubani yalilenga maeneo ya kambi ya kijeshi katika jimbo la Isfahan katikati mwa Iran. Shambulio hilo lilihusishwa Israel, ambayo hata hivyo haikudai kuhusika.

Diplomasia ya Iraq ilionyesha siku ya Ijumaa jioni "wasiwasi wake mkubwa" kuhusu shambulio la Isfahan na "kuonya juu ya hatari ya kuongezeka kwa uhasama ambao unatishia usalama na utulivu katika kanda hiyo". "Uhasama huu usiweze kugeikia kile kinachotokea katika Ukanda wa Gaza, uharibifu na watu wasio na hatia kupoteza maisha," diplomasia ya Iraq imesema.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.