Pata taarifa kuu
SUDAN KUSINI

Vikosi vya Machar vyakaribia mjini Juba

Msemaji wa vikosi vya upinzani nchini Sudan Kusini SPLA-IO James Gatdet Dak amesema vikosi hivyo vimefanikiwa kuvishinda vile vinavyomuunga mkono rais Salva Kiir karibu na mji mkuu Juba.

Vikosi vya Riek Machar wakiwa juu la Lori
Vikosi vya Riek Machar wakiwa juu la Lori Sudan News
Matangazo ya kibiashara

Gatdet ameongeza kuwa kwa sasa kinachosubiriwa ni vikosi hivyo vya upinzani kupata idhini kutoka kwa Kamanda wao kuingia jijini Juba kwa makabiliano zaidi na vikosi vya Kiir.

Msemaji huyo ameliambia jarida la Sudan Tribune kuwa, mamia ya wanajeshi wa Kiir wameuawa Magharibi, Kusini na Kaskazini mwa mji wa Juba.

Naye mwandishi wa RFI Kiswahili wa maswala ya Sudan Kusini James Shimanyula amethibitisha kutokea kwa mapigano hayo nje ya mji wa Juba.

“Kuna makabiliano makali pembezoni mwa mji wa Juba, lakini si mfululizo,” amesema.

“Vikosi vya Machar vitaingia Juba hivi karibuni,” ameongeza.

Wakati hayo yakijiri, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linathathmini uwezekano wa kuzuru nchi hiyo kuhimiza amani.

Sudan Kusini iliingia katika mapigano mapya mapema mwezi uliopita, baada ya wanajeshi wa rais Kiir na wale wa Machar aliyekuwa Makamu wa kwanza wa rais kuanza kukabiliana karibu na na Ikulu mjini Juba na kusababisha zaidi ya watu 300 kupoteza maisha.

Machar ameondoka jijini Juba na haijulikani yuko wapi.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, rais Kiir alimteua Jenerali Taban Deng Gai kuwa Makamu wa kwanza rais kuchukua nafasi ya Machar.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.