Pata taarifa kuu
SIASA TANZANIA

Magufuli ashinda tiketi ya kuwania urais kupitia chama cha CCM Tanzania

Waziri wa Ujenzi nchini Tanzania John Pombe Magufuli amechaguliwa kupeperusha bendera ya chama tawala CCM wakati wa uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba mwaka huu.

John Pombe Magufuli mgombea urais CCM
John Pombe Magufuli mgombea urais CCM
Matangazo ya kibiashara

Magufuli mwenye umri wa miaka 55, alimshinda Asha-Rose Migiro ambaye ni Waziri wa Katiba na Sheria na Amina Salum Ali, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Tume ya Umoja wa Afrika kwenye Umoja wa Mataifa nchini Marekani.

Wawili hao walifika katika hatua ya tatu bora na kupigiwa kura siku ya Jumamosi usiku na baadaye matokeo yakatangazwa siku ya Jumapili.

Akitangaza matokeo hayo, Spika wa bunge Anna Makinda alisema Magufuli alipata ushindi wa kura za wajumbe 2,104 sawa na asilimia 87.1, akifuatwa na Amina Salum Ali aliyepata kura 253 sawa na asilimia 10 nukta 5 huku Asha Migoro akimaliza wa tatu kwa kupata kura 59 sawa na asilimia 2 nukta 4.

Kwa ushindi huu, Magufuli ndiye atakayemenyana na mgombea wa upinzani na ikiwa atashinda atakuwa rais wa tano wa Tanzania baada ya rais Jakaya Kikwete.

Magufuli anayefahamika kwa umaarufu wake wa kutaja takwimu za Kilomita za barabara zilizotiwa lami, amewaambia wajumbe wa CCM kuwa atahakikisha kuwa anakiunganisha chama hicho na kufanya kampeni kuhakikisha kuwa chama hicho kinapata ushindi tarehe 25 mwezi Oktoba.

Wanasiasa 38 wa CCM waliomba nafasi ya kupeperusha Bendera ya chama hicho akiwemo aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowasa na Waziri wa Mambo ya nje Bernard Membe.

Siku ya Jumamosi kulikuwa na hali ya wasiwasi baada ya kuondolewa kwa jina la Lowassa ambaye alionekana kuwa na uungwaji mkono wa wananchi wengi, huku mpinzani wake Bernard Membe akifuzu kuwa katika tano bora.

Baada ya mshindi kupatikana, wajumbe waliohudhuria mkutano huo walionekana kuzungumza kwa sauti moja na kumuunga mkono Magufuli na kumpa jina “Jembe” litakalofanya kazi bila kuchoka.

Katika historia ya chama hicho, wanawake wawili walifika katika hatua ya mwisho huku waliojitokeza kuomba kupeperusha bendera ya chama hicho wakijitokeza kwa wingi.

Chama cha Mapinduzi ambacho kimekuwa kikiongoza nchi hiyo toka mwaka 1977 kimekuwa kikishinda uchaguzi nchini humo .

 

 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.