Pata taarifa kuu

Jiji la Khartoum latikiswa na milipuko katika mapigano kati ya Burhan na Daglo

NAIROBI – Milipuko mikubwa imeendelea kutikisa mji wa Khartoum wakati huu mapigano kati ya majenerali wanaohasimiana nchini Sudan yakionyesha kutotulia licha ya mazungumzo nchini Saudi Arabia.

Mapigano kati ya wanajeshi na wanamgambo yanaendelea mjini Khartoum licha ya mazungumzo kati ya pande hizo mbili nchini Saudi Arabia.
Mapigano kati ya wanajeshi na wanamgambo yanaendelea mjini Khartoum licha ya mazungumzo kati ya pande hizo mbili nchini Saudi Arabia. AP - Marwan Ali
Matangazo ya kibiashara

Wakazi wameripoti kuendelea kwa mapigano katika mji wa Khartoum, ambapo milio ya risasi imesikika kaskazini mwa Omdurman na mashariki mwa Bahri, miji hii miwili  inatenganishwa na mto Nile.

Vikosi vya RSF vimeshutumu jeshi la Sudan kwa kuanzisha mashambulio ya anga dhidi ya ikulu ya zamani ya rais wa nchi hiyo katika mji mkuu, Khartoum, ambapo wakaazi wa jiji hilo wamesema mashambulio hayo yameharibu jumba hilo, shutuma ambazo zimekanushwa na jeshi la nchi hiyo.

Tangu hapo jana, jeshi limekuwa likishambulia miji hiyo kwa lengo la kuviondoa vikosi vya RSF ambavyo vimechukua udhibiti wa eneo kubwa la makazi ya watu na maeneo ya kimkakati tangu kuanza kwa mapigano hayo mwezi uliopita.

Kufikia sasa hakuna mwafaka ambao umefikiwa licha ya mazungumzo yanayoendelea nchini Saudia, mazungumzo yatakayosaidia kumaliza vita kati ya jenerali Abdel Fattah Al-Burhan na Mohammed Hamdan Daglo, na kuleta afueni ya janga la kibinadamu.

Shirika la mpango wa chakula duniani WFP, limesema watu milioni 2.5 nchini Sudan, huenda wakakabiliwa na njaa katika miezi ijayo.

Wakati haya yakijiri mkurugenzi mkuu wa idara ya uhamiaji nchini Sudan Kusini, amesema kuwa nchi yake itaondoa ada za viza kwa raia wa kigeni wanaokimbia mzozo katika mpaka wake na nchi jirani ya Sudan.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Atem Marol Biar, amewaagiza maafisa wa uhamiaji katika maeneo yote ya kuvuka mpaka na Sudan kutotoza ada za viza kwa wageni.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.