Pata taarifa kuu
AFCON 2027

Kenya: Uwanja wa Moi Kasarani kukarabatiwa kwa maandalizi ya AFCON 2027

Nairobi; Kenya – Baada ya Kenya kushinda haki za kuandaa Kombe la Mataifa ya Afrika ya mwaka 2027, waziri wa michezo nchini Kenya Ababu Namwamba ametangaza rasmi kufungwa kwa uwanja wa Moi Kasarani kupisha ukarabati kuanza mara moja.

Uwanja wa kimataifa wa michezo wa Moi Kasarani jijini Nairobi nchini Kenya.
Uwanja wa kimataifa wa michezo wa Moi Kasarani jijini Nairobi nchini Kenya. © Wizara ya Michezo nchini Kenya
Matangazo ya kibiashara

Mwezi Septemba, Shirikisho la Soka barani Afrika CAF, lilitangaza Kenya, Uganda na Tanzania kuwa waandalizi rasmi wa toleo la 36 la mashindano hayo.

Ukarabati huu unatarajiwa kuchukua miezi kumi na mbili huku makataa ya CAF ya viwanja kuwa tayari ikiwa mwezi Januari mwaka 2025.

Kufikia wakati tutakapomaliza chini ya takriban miezi 18, Kasarani itakuwa uwanja mpya na itakuwa tayari kuandaa AFCON ’27 - Waziri wa Michezo Kenya, Ababu Namwamba.

Ababu Namwamba kwenye ziara ya ukarabati wa uwanja huo
Ababu Namwamba kwenye ziara ya ukarabati wa uwanja huo © Ministry of Sports Kenya

Uwanja wa Kasarani na uwanja mpya wa Talanta unaotarajiwa kujengwa jijini Nairobi ndizo zilichagulia kuwa nyuga rasmi za mashindano hayo.

Kampuni ya Uchina Giang Xi ndio wanakandarasi wa ujenzi huo ambao watafanyia maeneo yote ya uwanja ukarabati. Ila waziri Namwamba alitaja maeneo 24 muhimu ya kuboreshwa.

https://www.rfi.fr/sw/michezo/20231108-afrika-mashariki-yaanza-kujiandaa-afcon-2027

‘Muonekano Mpya wa Kimataifa?’

Sehemu ya mashabiki itafunikwa kwa kujenga paa iliyofumwa ili kutoa kivuli kukinga mashabiki na jua au mvua. Paa hii ambayo itawekwa uwanja mzima, ni yenye upana wa mita 32 huku katika maeneo mengine ikizidishwa kwa mita 20. Dari hiyo itatengenezwa kwa mfumo wa kisasa wa Teflon au PTFE.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi Patrick Mariru akiweka jiwe la msingi la ukarabati wa uga wa Kasarani
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi Patrick Mariru akiweka jiwe la msingi la ukarabati wa uga wa Kasarani © Wizara ya Michezo nchini Kenya

Taa za kisasa zenye uwezo wa kutoa mwangaza mara 2000 kwa vipimo zitawekwa ili kuwezesha mechi za usiku kuchezwa, kujenga lifti mbili mpya katika maeneo ya VVIP, kujenga kituo cha uendeshwaji wa shughuli zote za uwanja, kuweka vifaa viwili vya kielektroniki vya matokeo kusini na kaskazini mwa uwanja huo, kujenga upya vituo viwili vya wanahabari na kujenga eneo maalum la kamera ambalo litahudumu kama kitovu cha upeperushaji michuano.

Sura hii mpya inatarajiwa kuwekwa vifaa vya huduma ya kwanza katika kila maeneo ya uwanja kuanzia juu hadi chini. Vyumba vya wachezaji kubadilishia mavazi na vyoo pia vitajengwa upya wakati huu vikizingatia watu wanaoishi na ulemavu. Maeneo ya biashara ndogo ndogo ya kuuza vinywaji na vyakula wakati wa mechi zitajengwa pia.

Eneo la wageni mashuhuri linatarajiwa kupanuliwa na kuwekwa vifaa vya huduma ya kwanza. Eneo hili litajengwa kwa mbinu ya kisasa ya ‘Skyboxes’ – eneo lenya viti vya faragha vilivyo sehemu ya juu kabisa katika uwanja wa michezo na kwa kawaida huwa na huduma za kifahari. Sky Box ni sehemu yenye starehe na kwa kawaida huwa na lango tofauti kando na wageni kuwa na uwezo wa kuona uwanja mzima kwa mwonekano mmoja mfumo wa bakuli la uwanja.

Ababu Namwamba kwenye ziara ya ukarabati wa uwanja huo
Ababu Namwamba kwenye ziara ya ukarabati wa uwanja huo © Ministry of Sports Kenya

Mpango huo pia utashuhudia viwanja vyote kuwekwa zulia la mfumo wa ‘epoxy’, kujenga eneo la matibabu kwenye vyumba vya kubadilishia mavazi ambapo pia wataanzisha maeneo ya kufanyia vipimo vya matumizi ya dawa ya kusisimua misuli.

Kuboresha nyasi ya uwanja ambao pia utazingatia uwezo wa uwanja huo kukauka wakati wa mvua chini ya dakika sita. Vigezo ya CAF vinahitaji uwanja uwe na uwezo wa kukausha uwanja kwa kasi ya kati ya dakika sita au nane wakati wa mechi - kigezo ambacho uwanja wa Kasarani kwa sasa haujaafiki.

Eneo la timu zinazochuana kuingia uwanjani wakati wa mechi pia litafanyiwa marekebisho pamoja na ujenzi wa maeneo mapya ya benchi la ufundi.

“Uwanja huu pia utawekwa mfumo wa VAR ili mechi ziweze kuamuliwa kupitia njia za kidijitali,” alisema waziri Ababu Namwamba.

Viongozi wa Wizara kwenye majadiliano
Viongozi wa Wizara kwenye majadiliano © Wizara ya Michezo nchini Kenya

Televisheni za mauzo za kidijitali zinazozingira zulia la uwanja wakati wa mechi pia zitawekwa, maeneo mengine yote nje ya uwanja kama vile sehemu za kuegesha magari na nyua zitajengwa upya.

Mfumo mpya wa kidijitali wa tiketi za mashabiki utawekwa ambapo tiketi itakuwa na nambari maalum ya kiti cha shabiki. Uga huo pia utabadilishwa sura ya nje kwa kupakwa rangi upya pamoja na kujenga ukumbi mpya wa kufanyia mazoezi.

Idara ya usalama nchini Kenya itasimamia ukarabati huo, katibu mkuu wa michezo Peter Tum akitoa hakikisho ya uwanja huo kujisimamia baada ya AFCON ’27 katika suala la kuzalisha fedha za kudumisha hali ya uwanja.

Katibu mkuu wa wizara ya ulinzi Patrick Mariru pia alielezea imani yake katika mradi huo.

Wizara ya Ulinzi ndio itasimamia mradi huu. Kazi hii itamalizika kwa wakati na bajeti iliyootengwa.

Patrick Mariru na Ababu Namwamba uwanjani Kasarani
Patrick Mariru na Ababu Namwamba uwanjani Kasarani © Wizara ya Michezo nchini Kenya

Kabla ya kufungwa kwa uwanja huo, mechi ya kirafiki kati ya timu ya taifa ya Kenya ya wasichana na wavulana walio chini ya miaka 19, ilichezwa kama njia ya kupigia kwaheri kwa uwanja huo kabla ya kupata sura mpya.

Uwanja Mpya wa Talanta je?

 

Umbo la uwanja mpya wa Talanta unaotarajiwa kujenga jijini Nairobi, Kenya
Umbo la uwanja mpya wa Talanta unaotarajiwa kujenga jijini Nairobi, Kenya © Wizara ya Michezo nchini Kenya

 

"Uzinduzi rasmi wa ujenzi wa uga huo utafanywa na rais William Ruto mwenyewe. Ni mradi mkubwa na muhimu kwa serikali hii, sababu utakuwa uwanja wa kwanza wa kimataifa kujengwa tangu uwanja wa Moi Kasarani. Tumemuomba rais afanye uzinduzi na akiwa tayari tutawaalika wakenya," alisema Waziri Ababu Namwamba.

Aidha waziri aliondoa wasiwasi wa wakenya kuhusu ukarabati wa mara kwa mara kwani "sasa tuna uongozi mpya, azma mpya, mtindo mpya, mwelekeo mpya na wakenya watarajie matokeo mapya kwa sababu ni mwanzo tofauti."

Zimesalia siku 28 kabla ya Kombe la Mataifa ya Afrika ya mwaka 2024 kuanza nchini Ivory Coast.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.