Pata taarifa kuu

Kundi la Islamic State linadai kuhusika na milipuko miwili nchini Iran

Kundi la kigaidi la IS limedai kuhusika Alhamisi hii, Januari 4 kupitia ujumbe wa Telegraph kwa shambulio la mabomu mawili ambalo lilisababisha vifo vya zaidi ya watu 80 na karibu 300 kujeruhiwa siku moja kabla ya hafla ya kumuenzi Jenerali Qassem Soleimani, aliyeuawa na shambulizi la Marekani mnamo mwaka 2020.

Mwanamke akilia katika eneo la shambulio la mabomu mawili ambalo lilisababisha vifo vya watu zaidi ya 80 na karibu 300 kujeruhiwa siku moja kabla huko Kerman, Januari 4, 2024.
Mwanamke akilia katika eneo la shambulio la mabomu mawili ambalo lilisababisha vifo vya watu zaidi ya 80 na karibu 300 kujeruhiwa siku moja kabla huko Kerman, Januari 4, 2024. AP - Vahid Salemi
Matangazo ya kibiashara

Katika ujumbe wake uliochapishwa kwenye Telegram, kundi la Islamic State limebaini kwamba wapiganaji wake wawili "walibonyesza mkanda wao wa vilipuzi" katikati ya "mkusanyiko mkubwa wa waasi, karibu na kaburi la kiongozi wao "Qassem Soleimani" jana huko Kerman, kusini mwa Iran. Kundi hili la wanajihadi, ambalo linawachukulia Waislamu wa madhehebu ya Shia, walio wengi nchini Iran, kama waasi, lilijumuisha operesheni hii kama sehemu ya kampeni inayoitwa "Na waueni popote mtakapowapata", kulingana na taarifa kwa vyombo vya habari. Dakika chache kabla ya madai hayo, ISIS ilitoa rekodi ya sauti ya msemaji wake ikisema kwamba kampeni hii ilikuwa inafanywa "kuunga mkono Waislamu popote walipo, hasa Palestina".

Shambulio hilo lilitokea karibu na msikiti wa Saheb al-Zaman ambao ni kaburi la Jenerali Soleimani aliyeuawa mwezi wa Januari 2020 katika shambulio la ndege zisizo na rubani za Marekani nchini Iraq. Qassem Soleimani alikuwa mtu muhimu katika Jamhuri ya Kiislamu na mmoja wa watu mashuhuri zaidi wa nchi hiyo. Aliyetangazwa kuwa "shahidi aliye hai" na Ayatollah Ali Khamenei alipokuwa bado hai, Soleimani alisherehekewa kwa jukumu lake katika kushindwa kwa ISIS nchini Iraq na Syria.

Idadi ya awali ya vifo vya zaidi ya watu 100 ilirekebishwa na kupunguzwa siku ya Alhamisi na mkuu wa idara ya huduma za dharura nchini Iran, Jafar Miadfar, ambaye aliripoti watu 84 waliuawa na 284 kujeruhiwa. Hili ndilo shambulio baya zaidi kuwahi kutokea nchini humo tangu mwaka 1978, wakati shambulio la uchomaji moto lilipoua takriban watu 377 katika jumba la sinema huko Abadan, kulingana na kumbukumbu za shirika la habari la AFP.

Shambulio hilo likiwa limetokea katika mazingira magumu ya kikanda tangu kuanza kwa mzozo mwezi Oktoba kati ya Israel na Hamas, maafisa wa Iran mara moja walinyooshea kidole Israel na Marekani. Rais wa Iran Ebrahim Raissi alisema kuwa taifa la Kiyahudi litalipa gharama kubwa kwa uhalifu wake. Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani iliona "upuuzi" pendekezo lolote la kuhusika kwa Washington au Tel Aviv katika kile "kinachoonekana kama shambulio la kigaidi, aina ya kitu ambacho ISIS wamefanya huko nyuma", kulingana na afisa mkuu wa Marekani aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina.

Israel, adui mkubwa wa Iran, haijazungumza lolote kuhusu shambulio hilo. "Tumejikita kwenye mapigano na Hamas" katika eneo la Palestina la Ukanda wa Gaza, alisema msemaji wa jeshi la Israel Daniel Hagari.

(Pamoja na AFP)

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.