Pata taarifa kuu
SAUDI ARABIA-G20-CORONA-USHIRIKIANO

Mfalme Salman atoa wito kwa nchi za G20 kwa ushirikiano zaidi dhidi ya COVID-19

Viongozi wa nchi zenye nguvu kiuchumi duniani wanafanya mkutano kwa njia ya video kujadili namna ya kupambana na Corona na kuufufua uchumi wa dunia nchini Saudi Arabia.

Mfalme Salman akitoa hotuba wakati wa kikao cha ufunguzi wa Mkutano wa 15 wa Viongozi wa G20 huko Riyadh Jumamosi, Novemba 21.
Mfalme Salman akitoa hotuba wakati wa kikao cha ufunguzi wa Mkutano wa 15 wa Viongozi wa G20 huko Riyadh Jumamosi, Novemba 21. VIA REUTERS - BANDER ALGALOUD
Matangazo ya kibiashara

Mkutano huo ulifunguliwa Jumamosi hii na Mfalme Salman ambaye aliomba ushirikiano kati ya nchi za G20 kukabiliana na janga la COVID-19.

Wengi wameomba chanjo kupatikana haraka iwezekanavyo ili kudhibiti ugonjwa huu hatari ambao umesababisha vifo vingi duniani.

"Ulimwengu wote unatazama. Kwa hivyo lazima tuunde mazingira ya kupatikana kwa chanjo kwa bei rahisi na sawa kwa wote, " Mfalme Salman amesema.

Hoja ya Mfalme Salman imeungwa mkono na rais wa China Xi Jinping, ambaye ameahidi kuimarisha ushirikiano wa nchi yake katika utafiti, maendeleo, uzalishaji na usambazaji wa chanjo.

"Tutasaidia nchi zinazoendelea ili chanjo ziwe mali ya umma", ameongeza rais wa China.

Jambo lingine lililotawala mkutano huu ni msaada kwa nchi masikini na zenye mzigo mkubwa wa madeni. Nchi za G20 zimeamua kuidhinisha - kwa kuiongeza muda wa miezi sita hadi katikati ya mwaka 2021 - kusitishwa kwa malipo ya madeni kwa nchi zinazoendelea.

Mkuu wa Benki ya Dunia David Malpass amekaribisha makubaliano yaliyofikiwa, wakati akiwataka viongozi kwenda mbali zaidi katika kupunguza madeni, hasa kwa nchi za Afrika. "Changamoto ya madeni inaweza kuturudisha nyuma kutokana na hali ambayo tayari imezikumba nchi hizi kwa miaka thelathini iliyopita," amesema.

Suala la mabadiliko ya tabia nchi pia linatarajiwa pia kuwa mada kuu, huku mabadiliko ya uongozi wa Marekani yakiongeza matumaini ya juhudi za pamoja zaidi katika kiwango cha G20 za kupambana na ongezeko la joto duniani.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.