Pata taarifa kuu
MALI-MAUAJI

Kundi la Kigaidi la Al-Qaeda lakiri kuhusika na mauaji ya waandishi wa habari wawili wa Ufaransa waliouawa mwishoni mwa juma lililopita katika nchi ya Mali

Kundi la Al Qaeda tawi la ukanda wa Maghreb, limejigamba kuhusika katika mauaji ya waandishi wa habari wawili raia wa Ufaransa Novemba 2 mjini Kidal kaskazini mashariki mwa Mali na kudai kuwa ni ulipizaji kisasi kwa vitendo vya wanajeshi wa Ufaransa wanaowafanyia wenzao huko kaskazini mwa Mali. Katika taarifa iliotolewa na mtandao mmoja nchini Mauritania wa Sahara Medias, kundi la Al Qaeda eneo la Maghreb (Aqmi) limethibitisha kuwa mauaji hayo yametekelezwa ili kujibu mapigo ya maumivu wanayoyapata raia wa Mali kutoka kwa wanajeshi wa Ufaransa na wale Umoja wa Afrika katika eneo la Azawad.

RFI, Novemba 5, 2013
RFI, Novemba 5, 2013 ©Pierre René-Worms
Matangazo ya kibiashara

Kundi hilo la Aqmi linachukulia mauaji hayo kama bili ambayo inatakiwa kulipwa na Rais wa Ufaransa Francois Hollande na watu wake katika mapambano ya kidini ilioanzisha huko Mali.

Kulingana na kituo cha sahara Medias, Umoja wa wawapiganaji wa kundi la Aqmi uliotekeleza mauajo hayo ni kundi la Abdelkarim Targui, raia wa Tuareg aliyekuwa karibu sana na kiongozi wa kundi la Aqmi Abou Zeid aliyeuwawa mwanzoni mwa Mwaka huu wakati wa operesheni ya majeshi ya Ufaransa na Tchad katika milima ya Ifoghas.

Ghislaine Dupont mwenye umri wa miaka 57 na Claude Verlont mwenye umri wa miaka 55 waandishi wa habari wa RFI waliuawa katika eneo la kilometa chache na mji wa Kidal muda mfupi baada ya kutekwa na kundi ndogo la watu waliokuwa wamejihami kwa silaha.

Polisi wa Ufaransa wapo nchini Mali katika juhudi za kuwasaka waliotekeleza mauaji hayo.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande amesema jana katika kikao cha baraza la mawaziri kwamba Uchunguzi tayari umepiga hatua kubaini wahusika, na kusema kuwa wanafanya kila jitihada kuhakikisha wahusika wanakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Taarifa hiyo ya Ikulu ya rais nchini Ufaransa kupitia msemaji wa serikali Najat Vallaud-Belkacem imesema rais Hollande ameendelea kueleza maskitiko yake kutoka na vifo hivyo vya waandishi wa habari wa RFI na kubaini kuwa sio raia wa Ufaransa pekee waliolengwa, lakini pia uhuru wa kujitetea.

Matamshi haya ya rais Hollande yanathibitisha taarifa iliyotolewa jana ya kukamatwa kwa watu 35 wanaoshukiwa kuhusika na mauaji hayo.

Taarifa zaidi kutoka mjini Kidal zimearifu kuwa ndani ya gari ilioachwa karibu na eneo la mauaji, kumegundulika namba muhimu za simu ambazo zitasaidia katika kuendesha uchunguzi.

Duru nyingine iliyo karibu na utawala wa Mali imearifu kuwa kundi la watu waliowateka waandishi hao wa habari kwa ajili ya manufaa ya kundi la Aqmi baadhi ya wafuasi wa kundi hilo wapo jela kufuatia tukio kama hilo la kuwateka wafaransa mwaka 2011, na hii itasaidia pia katika uchunguzi.

Mwezi Novemba mwaka 2011, wafaransa wawili Philippe Verdon ambaye aliuawa na Serge Lazatevic ambaye bado anashikiliwa na kundi la magaidi walitekwa na kundi moja kwa faida ya kundi la Aqmi katika eneo la Hombori kaskazini mwa Mali. Baadhi ya wafuasi wa kundi hilo walikamatwa na kusafirishwa jijini Bamako.

Shughuli za kutoa heshima kwa waandishi hao wa habari hao zilizotangwazwa duniani kote kupitia RFI zilifanyika jana jijini Paris wakiwepo pia viongozi wa Radio pamoja na washirika wao, wanadiplomasia, na wanasiasa wa Mali.

Hisia na huzuni ziliwapata waliokuwepo katika shughuli hizo pale iliposikilizwa ripoti ya marehemu Ghislaine Dupont, ambaye ambaye alikuwa maharufu sana duniani hususan barani Afrika.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.