Pata taarifa kuu
URUSI-SYRIA-MAREKANI-UINGEREZA

Urusi: Kuishambulia Syria kijeshi ni hatari kwa nchi jirani na kutachochea ugaidi mashariki ya kati

Serikali ya Urusi hii leo imeonya kuhusu kile ambacho imekiita kukua na kukithiri kwa vitendo vya ugaidi kwenye eneo la ukanda wa mashariki ya kati, iwapo Marekani na washirika wake wataishambulia Syria kijeshi.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Syria, Walid al-Muallem (kushoto) akiwa na mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov (kulia)
Waziri wa mambo ya kigeni wa Syria, Walid al-Muallem (kushoto) akiwa na mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov (kulia) Reuters
Matangazo ya kibiashara

Kauli ya Urusi inatolewa wakati huu ambapo shinikizo zaidi linaongezeka kwa Serikali ya rais Bashar al-Assad licha ya Serikali yake kusisitiza kuwa iko tayari kwa mazungumzo na waasi wa Syria kumaliza machafuko nchini humo.

Akizungumza na wanahabari mjini Moscow mara baada ya kumaliza mazungumzo yake na waziri wa mambo ya Kigeni wa Syria, Walid al-Muallem, waziri wa mambo ya nje Sergei Lavrov ameonya kuhusu uwezekano wa mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Syria.

Waziri Lavrov amesema kuwa kuivamia kijeshi nchi ya Syria kutatoa mwanya wa kuongezeka kwa makundi ya kigaidi nchini humo kwakuwa hata sasa hakuna utawala rasmi wa waasi kwakuwa kuna makundi ambayo tayari yamejianisha kuwa na uhusiano na mtandao wa kigaidi duniani wa Al-Qaeda.

Waziri Lavrov ameongeza kuwa iwapo kutafanyika mashambulizi yoyote ya kijeshi dhidi ya Syria, ni wazi nchi ya Syria itatumbukia kwenye vita vya wenyewe na kuhatarisha usalama wa nchi jirani pamoja na eneo zima la mashariki ya kati.

Urusi inasisitiza kuwa mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Syria sio suluhu la mzozo wa Syria bali juhudi za kisiasa na mazungumzo ndio mbinu pekee zinazoweza kumaliza tofauti ya kisiasa nchini Syria.

Kwa upande wake, waziri Muallem ametetea nchi yake akisema wanajeshi wao hawakutumia silaha za kemikali na kwamba huu ni mpango wa Marekani na washirika wake kutaka kutafuta kibali feki cha kuuangusha utawala wa rais bashar al-Assad jambo ambalo hawako tayari kuliona likitokea.

Kauli ya waziri Lavrov inakuja wakati huu ambapo waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Uingereza William Hague wakifanya mkutano wa pamoja mjini London kuzungumzia mzozo wa Syria na kukosoa msimamo wa Urusi na utawala wa rais Assad.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.