Pata taarifa kuu
TANZANIA-UFARANSA

Ufaransa ya ahidi kuongeza misaada zaidi kwa Tanzania na nchi za ukanda

Ufaransa imesema itaendelea kushirikiana kwa ukaribu na Serikali ya Tanzania hasa katika masuala yanayohusu maendeleo, na kwamba imeridhishwa na kasi ya ukuaji wa uchumi wa taifa hilo pamoja na kupongeza hatua ambazo zimeendelea kuchukuliwa na Rais John Pombe Magufuli.

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa, Jean-Marc Ayrault, akizungumza kwenye mahojiano maalumu na rfikiswahili, Agosti 2, 2016.
Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa, Jean-Marc Ayrault, akizungumza kwenye mahojiano maalumu na rfikiswahili, Agosti 2, 2016. Emmanuel Makundi/RFI
Matangazo ya kibiashara

Akizungumza jijini Dar es Salaam, kwenye mahojiano ya kipekee na idhaa hii ya kiswahili ya radio France International, waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa, Jean-Marc Ayrault, amesema ziara hii ni ya kwanza kuifanya kwa nchi ya Tanzania, na amekuja kutoa hakikisho la Serikali yake kwa Tanzania.

Jean-Marc Ayrault, ameongeza kuwa, kumekuwa na dhana potofu kuhusu ushirikiano wa nchi ya Ufaransa na mataifa ya Afrika na kwamba imekuwa ikiyasaidia mataifa yanayozungumza lugha ya kifaransa, dhana ambayo anasema ziara yake nchini Kenya na Tanzania, imeonesha wazi kuwa nchi yake inathamini mchango wa mataifa ya ukanda wa Afrika Mashariki pamoja na zile nchi ambazo hazizungumzi kifaransa.

Waziri Ayrault amesema, nchi yake inaamini kukua na kuimarika kwakekunategemea sana ushirikiano na nchi za Afrika na kwamba ndio maana ametembelea nchi ya Kenya na Tanzania kutoa hakikisho.

Waziri Jean-Marc Ayrault, amesema nchi yake kupitia shirika la misaada ya maendeleo la Ufaransa, AFD, litaongeza mara mbili zaidi msaada wake wa kifedha kwa nchi ya Tanzania, ambapo toka mwaka jana limekuwa likitoa msaada wa zaidi ya dola za Marekani milioni 100, kusaidia miradi ya maji, nishati, miundo mbinu na usafiri.

Mbali na kuzungumzia misaada ya nchi yake kwa Tanzania, waziri, Ayrault, amepongeza hatua zinazochukuliwa na rais Magufuli katika kuimarisha utawala bora na uwajibikaji, pamoja na kujenga ushirikiano mzuri na nchi wanachama za jumuiya ya Afrika Mashariki.

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa, Jean-Marc Ayrault.
Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa, Jean-Marc Ayrault. Emmanuel Makundi/RFI

Kuhusu mizozo kweye eneo la nchi za maziwa makuu, waziri, Ayrault, amesisitiza utayari wa nchi yake kuendelea kushirikiana na wadau wa ukanda katika kuhakikisha suluhu inapatikana hasa kwenye nchi ambazo zimekumbwa na machafuko.

Amesema Ufaransa itaendelea kuweka shinikizo kwa nchi ya Burundi kukubali kuwapokea askari polisi wa kulinda amani ambao watapelekwa nchini humo, kwa lengo la kuhakikisha usalama wa raia na kuzuia kuendelea kushuhudiwa kwa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu vinavyodaiwa kutekelezwa na pande zinazokinzana nchini humo.

Kuhusu uchaguzi mkuu wa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya kongo DRC, waziri Jean-Marc Ayrault, ametoa wito kwa Serikali iliyopo madarakani kuheshimu katiba ya nchi ya kufanya uchaguzi ndani ya muda uliopangwa ili kuepusha machafuko ya kisiasa yanayoweza kutokea.

Jean-Marc Ayrault, pia amezungumzia kinachoendelea kwenye nchi ya Sudan Kusinim ambapo amesema njia pekee ya kumaliza machafuko yanayoshuhudiwa kwa sasa ni kwa viongozi wa nchi hiyo kujua wajibu wao, na kukubali kutekeleza kwa uaminifu mkataba wa amani uliotiwa saini hivi karibuni.

Akiwa nchini Kenya, waziri Jean-Marc Ayrault, ameihakikishia nchi yake kuwa, nchi yake itaendelea kuisaidia katika kupambana na vitendo vya kigaidi, hasa makundi ya kiislamu kama vile Al-Shabab na Al-Qaeda, makundi ambayo amesema yamekuwa hatari sio tu kwa usalama wa Kenya na Ufaransa bali kwa usalama wa dunia.

Amesema nchi yake itaendelea kutoa msaada wa hali na mali katika kuimarisha sekta ya usalama na hasa katika kubadilishana taarifa za kiintelijensia kuhusu washukiwa wa Ugaidi na tishio lolote la ugaidi kwa nchi za ukanda.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.