Pata taarifa kuu

Kenya: Mkuu wa majeshi ya ulinzi Jenerali Francis Ogolla amefariki katika ajali

Rais wa Kenya, William Ruto katika hotuba yake taifa usiku wa Alhamis, amethibitisha kufariki kwa mkuu wa majeshi ya ulinzi katika taifa hilo Jenerali Francis Ogolla katika ajali ya helikopta ya kijeshi iliotokea saa nane mchana kwa saa za Nairobi.

Rais wa Kenya William Ruto wakati akiwa na mkuu wa majeshi ya ulinzi ya Kenya, Francis Ogolla jijini Nairobi.
Rais wa Kenya William Ruto wakati akiwa na mkuu wa majeshi ya ulinzi ya Kenya, Francis Ogolla jijini Nairobi. REUTERS - Monicah Mwangi
Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa rais Ruto, Jenerali Ogolla alikuwa kwenye helikopta hiyo pamoja na wanajeshi wengine kumi na mmoja ambapo ni watu wawili peke walioripotiwa kunusurika.

Ajali hiyo imetokea katika mpaka wa kaunti za Elgeyo Marakwet na Pokot Magharibi kilomita 400 kaskazini-magharibi mwa jiji kuu la Nairobi.

Aidha rais Ruto katika hotuba yake kwa taifa, amesema kuwa mkuu wa majeshi ya ulinzi Jenerali Francis Ogola alikuwa ameondoka Nairobi leo asubuhi ilikutembelea wanajeshi waliotumwa Kaskazini mwa mkoa wa bonde la ufa kwenye taifa hilo chini ya operesheni maliza uhalifu na pia kukagua miradi nyengine ya serikali ikiwemo kufunguliwa kwa shule zilizokuwa zimefungwa kutokana na utovu wa usalama unaotekelezwa na wezi wa mifugo.

Kwa mujibu wa rais Ruto, ndege iliokuwa imembeba kiongozi huyo wa jeshi ilianguka muda mfupi baada ya kupaa wakati wakitarajia kusafiri kuelekea eneo lengine.

Wezi wa mifugo wamekuwa wakiendelea kutatiza usalama wa raia katika mkoa wa bonde la ufa ambapo shule zimelazimika kufungwa kutokana na mashambulio ya wezi wa mifugo ambao pia wamesababisha vifo vya raia wa kawaida na maofisa wa usalama.

Jenerali Ogolla aliteuliwa na rais Ruto mwezi Aprili mwaka wa 2023, baada ya kuwa Kamanda wa jeshi la wanahewa na naibu mkuu wa majeshi ya Ulinzi.

Rais Ruto pia ametangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa ambapo bendera zote katika maeneo ya umma zitaperushwa nusu mlingoti.

Tayari viongozi mbalimbali wanaendelea kutuma pole zao kufuatia kifo cha mkuu wa huyo wa majeshi ya ulinzi.

Hillary Ingati, RFI-Kiswahili Nairobi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.