Kenya: Upinzani wamuonya balozi wa Marekani kuhusu uchaguzi uliopita
Nairobi – Viongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya, Azimio, wamemjia juu balozi wa Marekani nchini humo, Meg Whitman, ambaye wakati wa kongamano la ugatuzi alidai uchaguzi uliopita ulikuwa huru na haki akikosoa uchochezi wa vurugu.
Imechapishwa:
Kiongozi wa upinzani Raila Odinga wakati akihutubia kongamano hilo mjini Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu katika mkoa wa bonde la ufa siku ya Alhamisi, alimkashifu Whitman kwa kile alichodai kuwa anaingilia masuala ya Kenya.
Mkuu huyo wa upinzani alimwambia mjumbe huyo wa Marekani alipokuwa akitetea maandamano ya hivi majuzi ambayo alisema yalitimiza madhumuni ya kuunganisha nchi na kulazimisha serikali kuja kwenye meza ya mazungumzo.
Kinara wa muungano huo, Raila Odinga, sasa anamtaka balozi Meg kukaa kimya ama vinginevyo watashinikiza arudishwe nchini mwake.
“Waache Wakenya walivyo, kama maandamano yanaweza kusababibisha mazungumzo kati ya Ichung`wah na Kalonzo basi maandamano ni mazuri, Kenya sio Marekani au mkoloni mwa Marekani, funga mdomo wako ukiwa hapa hali si hivyo tutashinikiza urejeshwe kwenu.” alisema Odinga.
Raila Odinga kuhusu balozi wa Marekani
Aidha Odinga alisisitiza kuwa iwapo Whitman ataendelea kutoa maoni yake kuhusu masuala ya Kenya, basi huenda mrengo wa kisiasa wa upinzani ukalazimika kuiomba serikali ya Marekani kumuondoa kwenye taifa hilo.
Matamshi yake Odinga yanajiri baada ya yale ya wabunge wa upinzani ambao walimkashifu balozi huyo, huku baadhi yao wakimsihi abatilishe maoni yake ambayo walisema yalikuwa kinyume na uungaji mkono wa Marekani kwa demokrasia.
Wabunge hao pia walidai kuwa matamshi ya Whitman yanaweza kudhoofisha mazungumzo ya kitaifa yanayoendelea kati ya serikali na upinzani.