Upinzani nchini Kenya wasema umekubaliana na serikali kuzungumza
Muungano wa upinzani nchini Kenya, Azimio la Umoja, umesema umekubaliana na serikali, kuunda kamati ya watu 10 ili kujadili na kutatua changamoto zinazoikabili nchi hiyo.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Taarifa hiyo imetolewa Jumamosi jioni hii na kiongozi wa muungano wa upinzani bungeni, Opiyo Wandayi, ambaye amefafanua kuwa, maafikiano hayo yamekuja baada ya kushauriana na wenzao wa muungano wa Kenya Kwanza.
Aidha, Wandayi ameeleza , mazungumzo hayo yataongozwa na kusimamiwa na rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo, na yanalenga kutatua changamoto kati ya serikali na upinzani kwa manufaa ya wananchi wa Kenya.
Kila upande utatoa watu watano, kuunda kamati hiyo. Taarifa hiyo pia imethibitishwa na upande wa serikali, kupitia kiongozi wake bungeni, Kimani Ichung'wah.
Hata hivyo, haijafahamiki ni lini mazungumzo hayo yataanza.
— Kimani Ichung’wah (@KIMANIICHUNGWAH) July 29, 2023
Kauli hii ya upinzani inakuja baada ya wiki kadhaa za maandamano kupinga sheria ya fedha, iliyosababisha kupanda kwa gharama ya maisha. Maandamano hayo yalisababisha vifo vya watu zaidi ya 30 na mamia kujeruhiwa kwa mujibu wa mashirika ya Kimataifa ya kutetea haki za binadamu nchini humo.
Wiki hii Odinga alidokeza kuwa, rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alijaribu kumpatanisha na Ruto bila mafanikio huku rais William Ruto akisema yuko tayari kwa mazungumzo.