Wakenya wanamatumaini ya kumalizika kwa maandamano ya upinzani
Nairobi – Raia wa Kenya wameelezea matumaini yao ya kumalizika kwa mzozo wa kisiasa ambao umelikumba taifa hilo la Afrika Mashariki baada ya rais kusema kwamba yuko tayari kufanya kikao na kiongozi wa upinzani Raila Odinga wakati “wowote.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Waziri mkuu wa zamani Raila Odinga, aliitisha maandamano mwezi Machi ambapo hadi sasa mrengo wake umeshirki maandamano kwa siku tisa dhidi ya utawala wa rais Ruto.
Maandamano hayo yamegubikwa na machafuko pamoja na makabiliano makali baina ya wafuasi wa upinzani na maofisa wa polisi nchini humo.
Kupitia ukurasa wake wa twitter rais Ruto, ameonyesha nia yake ya kufanya mazungumzo na Odinga.
My friend @RailaOdinga ,am off to Tanzania for a human capital meeting to harmonise the expansion of employment opportunities in our continent. Am back tomorrow evening, and as you have always known, am available to meet one on one with you anytime at your convenience.
— William Samoei Ruto, PhD (@WilliamsRuto) July 25, 2023
WsR
Hadi tukichapisha taarifa hii, Odinga ambaye amewataka Wakenya kujitokeza kwa mkesha siku ya Jumatano kwa ajili ya kuwakumbuka waandamanaji waliouawa kwenye maandamano hayo, hajazungumzia wito wa mkuu wa nchi.
Vurugu hizo zimezua hasira miongoni mwa makundi ya kutetea haki za binadamu, polisi wakituhumiwa kwa kurusha mabomu ya machozi na risasi za moto kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wakirusha mawe.
Watu 20 wameuawa, kulingana na takwimu rasmi, ingawa Azimio (upinzani) unasema angalau watu 50 wamekufa.
Baadhi ya raia nchini humo haswa wafanyibiashara wanasema maandamano hayo yanatatiza biashara zao wakati baadhi ya wafuasi wa upinzani wakiwa na mtazamo tofauti.
Odinga, ambaye anadai uchaguzi wa urais wa mwaka jana ulikarabatiwa ameilaumu serikali kwa kupanda kwa gharama ya maisha ambapo pia amewatuhumu maofisa wa polisi na serikali kwa ukatili dhidi ya waandamanaji.