Kenya : Niko tayari kwa mazungumzo na upinzani : Rais Ruto
Nairobi – Rais wa Kenya William Ruto amesema, yupo tayari kukutana na kuzungumza na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, wakati wowote baada ya wiki kadhaa za maandamano dhidi ya serikali yake, na kusababisha maafa na majeruhi yanayoripotiwa kutekelezwa na polisi.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Ruto amemwambia Odinga kuwa, yupo tayari kukutana na Odinga.
My friend @RailaOdinga ,am off to Tanzania for a human capital meeting to harmonise the expansion of employment opportunities in our continent. Am back tomorrow evening, and as you have always known, am available to meet one on one with you anytime at your convenience.
— William Samoei Ruto, PhD (@WilliamsRuto) July 25, 2023
WsR
Hatua hii ya Ruto imekuja baada ya Odinga hapo jana kusema kuwa, kulikuwa na jitihada za kumpatanisha na Ruto chini ya rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan wiki mbili zilizopita, lakini juhudi hizo ziligonga mwamba.
‘‘Kumekuwa na jitihada kutoka nje kuona iwapo kuna uwezekano wa kufanyika kwa mazungumzo na sasa naweza kusema wazi hapa kwamba rais wa Tanzania alikuwa hapa wiki mbili zilizopita baada ya kualikwa na rais Ruto kujaribu kutusaidia katika mazungumzo lakini akasubirishwa na upande wa rais Ruto kwa siku mbili.’’
Kinara wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga
Odinga anasema hatua hiyo ya serikali ilichangia kuondoka kwa rais wa Tanzania nchini humo bila ya kukutana na viongozi hao.
Upinzani ambao umekuwa ukiitisha maandamano kulalamikia kupanda kwa gharama ya maisha nchini humo, umesitisha maandamano yaliyokuwa yafanyike leo kote nchini na badala yake imesema siku hii itatumiwa kuwaomboleza watu waliouawa mikononi mwa polisi.
Tayari shirika la kutetea haki za binadamu nchini humo, KNCHR, ambalo lilibuniwa na bunge, limesema linasikitisha kushuhudia ukiukaji wa haki za binadamu kutoka kwa waandamanaji waharibifu na polisi.
Wiki iliyopita, shirika la Amnesty International, lilishtumu kile lilitaja kuwa ukandamizaji kutoka kwa polisi na kusema walikuwa na ushahidi wa mauaji ya watu 27 katika mwezi Julai pekee.
Wakosoaji wanamtuhumu Ruto kuenda kinyume cha ahadi alizozitoa wakati kampeni za uchaguzi wa Agosti mwaka uliopita, alipoahidi kuimarisha uchumi na maisha ya wakenya kupitia mfumo wa kuwainua raia wa chini maarufu kama Bottom up.