Pata taarifa kuu

Kenya: Upinzani wapanga kuipeleka serikali ICC

NAIROBI – Kinara wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga, amesema muungano wao wa Azimio la Umoja-One Kenya, unaendelea kukusanya ushahidi ambao itauwasilisha katika mahakama ya ICC, kuonesha namna serikali inatumia vyombo vya usalama kunyanyasa na kuua raia wanaoshiriki maandamano ya amani.

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga, akizungumza  na wanahabari wa idhaa za kimataifa jijini Nairobi, Kenya, Tuesday, 25, July, 2023.
Kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga, akizungumza na wanahabari wa idhaa za kimataifa jijini Nairobi, Kenya, Tuesday, 25, July, 2023. AP - Khalil Senosi
Matangazo ya kibiashara

Aidha Odinga, amesema bado yuko tayari kukutana na rais William Ruto kuangalia namna atashughulikia madai yao, hata hivyo akimtuhumu kukaidi wito wa viongozi wa ukanda wanaojaribu kuwapatanisha.

Sasa naweza kusema hapa wazi kwamba rais wa Tanzania alikuja hapa wiki mbili zilizopita, baada ya kualikwa na rais Ruto ili kujaribu kutusaidia katika mazungumzo lakini alilazimishwa kusubiri kwa muda mrefu na baadaye akaamua kuondoka.

Odinga ameyasema haya hivi leo alipozungumza na vyombo vya habari vya kimataifa jijini Nairobi, na hii ni baada ya ukimya wa karibu wiki moja tangu maandamano ya wiki iliyopita, maandamano ya kulalamikia gharama ya juu ya maisha.

Tangu mwezi Machi mwaka huu, Muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya, umeandaa mikutano tisa ya maandamano dhidi ya serikali ya rais Ruto, katika maandamano ambayo waandamanaji na vikosi vya usalama wamekuwa wakikabiliana.

Polisi na magenge ya kulipwa wamewapiga risasi na kuwaua au kuwajeruhi raia wengi” amesema Odinga akiongeza kuwa vurugu hizo zililenga haswa kabila lake.

Wiki iliyopita, Ruto aliipongeza idara ya polisi jinsi ilivyoendesha shughuli zake wakati wa maandamano, akisema hatakubali kuwepo kwa vurugu, mapigano au uharibifu wa mali.

Yasemavyo mashirika ya haki za kibinadamu

Shirika la kutetea haki za binadamu nchini humo, KNCHR, ambalo lilibuniwa na bunge, limesema linasikitisha kushuhudia ukiukaji wa haki za binadamu kutoka kwa waandamanaji waharibifu na polisi.

Vikosi vya usalama jijini Nairobi wakati wa maandamano, Julai 20, 2023.
Vikosi vya usalama jijini Nairobi wakati wa maandamano, Julai 20, 2023. AFP - SIMON MAINA

Kadhalika, wiki iliyopita, shirika la Amnesty International, lilishtumu kile lilitaja kuwa ukandamizaji kutoka kwa polisi na kusema walikuwa na ushahidi wa mauaji ya watu 27 katika mwezi Julai pekee.

Upinzani wasitisha maandamano

Maandamano yalikuwa yametangazwa kufanyika Jumatano ya wiki hii, yalisitishwa, upinzani ukisema utatumia fursa hiyo kuwaomboleza waliouawa katika kipindi cha maandamano, kwa kuwasha mishumaa, na kuandaa maua meupe ili kuwakumbuka.

Wakosoaji wanamtuhumu Ruto kuenda kinyume cha ahadi alizozitoa wakati kampeni za uchaguzi wa Agosti mwaka uliopita, alipoahidi kuimarisha uchumi na maisha ya wakenya kupitia mfumo wa Bottom up.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.