Pata taarifa kuu

Kenya: Shughuli zaanza kurejea kawaida jijini Nairobi

Baadhi ya shughuli zilizokuwa zimeathirika hapo jana Jumatano nchini Kenya kwa hofu ya kutokea kwa maandamano ya upinzani zimeonekana kurejelewa hii leo ikiwemo maduka kufunguliwa na shule katika baadhi ya sehemu kufunguliwa.

Jumatano polisi walikabiliana na waandamanaji katika maeneo tofauti ikiwemo Nairobi
Jumatano polisi walikabiliana na waandamanaji katika maeneo tofauti ikiwemo Nairobi REUTERS - THOMAS MUKOYA
Matangazo ya kibiashara

Watu wawili walifariki Jumatano, ikiwa ni siku ya pili kati ya siku tatu za maandamano yaliyoitishwa wiki hii na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, mamlaka nchini humo zikisema zaidi ya watu 300 wamekamatwa.

Shule jijini Nairobi na ngome za upinzani mjini Kisumu na Mombasa zilifunguliwa Alhamisi, huku wizara ya mambo ya ndani ikiwahakikishia Wakenya kwamba ilikuwa imechukua "hatua za kutosha kuhakikisha usalama wa raia na wanafunzi".

Shughuli za kibiashara zimeonekana kuaanza kurejea jijini Nairobi baada ya kuathirika siku ya Jumatano huku maduka yakifunguliwa tena na wafanyikazi wakionekana kurejea katika sehemu zao za kazi.

Polisi wametumia gesi ya kutoa machozi na risasi za moto kutawanya umati wa watu waliokuwa wakirusha mawe, jambo lililozua ghadhabu kutoka kwa makundi ya kutetea haki za binadamu, huku watu wawili wakiuawa kwa kupigwa risasi Jumatano mjini Kisumu, kulingana na afisa wa hospitali moja katika eneo hilo.

Magazeti kuu yalichapisha tahariri ya pamoja siku ya Alhamisi yakimtaka Odinga na Rais William Ruto wafanye mazungumzo.

Ni mara ya tatu mwezi huu kwa Odinga kuandaa maandamano makubwa dhidi ya serikali anayosema si halali na kuituhumu kutokana na kupanda kwa  gharama ya maisha.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.