Pata taarifa kuu

Bahari ya Pasifiki: Wasiwasi watanda katika nchi kadhaa kutokana na 'El Niño'

Ofisi ya Hali ya Hewa ya Australia imetangaza Jumanne Septemba 19 kuwepo kwa mfumo wa hali ya hewa unaojulikana kama El Niño, ambao kwa ujumla unahusishwa na kuongezeka kwa joto na ukame mkubwa unaoweza kusababisha moto mbaya wa misitu. 

Katika mitaa iliyojaa mafuriko ya Esmeraldas, Ecuador, Juni 5, 2023. Mfumo wa hali ya El Niño inasababisha mvua kubwa na mbaya sana nchini mwaka huu.
Katika mitaa iliyojaa mafuriko ya Esmeraldas, Ecuador, Juni 5, 2023. Mfumo wa hali ya El Niño inasababisha mvua kubwa na mbaya sana nchini mwaka huu. AP - Cesar Munoz
Matangazo ya kibiashara

Australia inatarajia "moto zaidi kuliko wastani" wa majira ya joto ya kusini na inahofia kuzuka kwa moto mkubwa. Siku ya Jumatatu, Ecuador ilitangaza tahadhari ya rangi ya chungwa kutokana na "kukaribia" kuwasili kwa El Niño, ambayo inaweza kusababisha mvua kubwa.

Wasiwasi unaongezeka katika Pasifiki kufuatia mabadiliko ya tabianchi. Mnamo mwezi Julai, Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) lilikadiria uwezekano wa kutokea kwa jambo hilo katika kipindi cha pili miezi sita ya mwaka 2023 kwa 90% na tahadhari zinaongezeka.

Ecuador ilitoa ishara kuanzia Jumatatu kwa kutoka kwenye tahadhari ya manjano kwenda tahadhari ya rangi ya chungwa kutokana na "kukaribia" kuwasili kwa mfumo wa hali ya hewa unaojulikana kama El Niño. "Hii ina maana kwamba Ecuador inatoka hatua ya kuzuia hadi hatua ya maandalizi (...) Ili kufanya hivyo, tumepata ufadhili wa kimataifa wa zaidi ya dola milioni 500," alisema Rais Guillermo Lasso kwenye mtandao wa kijamii wa X (zamani ukiitwa Twitter).

Kulingana na Mkuu wa Nchi, fedha zitakazopatikana zitatumika "kushughulikia dharura ya barabarani, kununua mashine nzito (...) na kupata mita 1,200 za madaraja ya muda". "Kuwepo kwa tukio hilo la asili kumekaribia na kunaweza kuambatana na msimu wa mvua nchini humo katika kipindi cha pili cha miezi sita ya mwaka huu," ametangaza kwa upande wake Katibu wa shirika linalosimamia majanga, Cristian Torres, aliyenukuliwa katika taarifa ya rais.

Ecuador tayari imekumbwa na ongezeko la joto la mara kwa mara la maji ya Pasifiki. El Niño huleta mvua kubwa nchini, ambayo husababisha mafuriko mabaya na maporomoko ya ardhi. Serikali inahofia uharibifu mwaka huu sawa na ule wa mwaka 1997 na 1998, ambapo karibu watu 300 walikufa na hasara ilifikia karibu dola bilioni 3.

Tangu kuanza kwa mwaka huu, mvua tayari imesababisha vifo vya karibu watu mia moja nchini Ecuador. Na katika nchi jirani ya Peru, El Niño tayari inajifanya kuhisiwa na mvua kubwa, ukame na theluji ambayo imedhoofisha uchumi katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

Australia inahofia moto kuwa mbaya kama miaka mitatu iliyopita

Australia, kwa upande wake, inatarajia msimu wa joto. Leo Jumanne, Karl Braganza, mtabiri wa serikali, amesema mfumo wa hali ya hewa unaojulikana kama El Niño umetokea katika Bahari ya Pasifiki, sanjari na wimbi lisilo la kawaida la msimu wa joto linaloathiri mashariki mwa nchi kwa sasa. Kulingana mtabiri huyo, El Niño itachangia katika kuongeza joto baharini, huku bahari zikishuhudia viwango vya joto vilivyorekodiwa tangu mwezi Aprili. "Msimu huu wa kiangazi utakuwa na joto kali kuliko wastani na kwa hakika joto zaidi kuliko miaka mitatu iliyopita," ameonya.

"Kuwasili kwa El Niño kutaongeza kwa kiasi kikubwa uwezekano wa kuvunja rekodi za joto na kuchochea joto kali zaidi katika maeneo mengi ya dunia na katika bahari," katibu mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani, Petteri Taalas, alisema mwezi Julai.

Kulingana na mwanasayansi wa hali ya hewa Andrew King wa Chuo Kikuu cha Melbourne, El Niño huongeza hatari ya moto na ukame katika baadhi ya sehemu za Australia: "Hali ya hewa ya joto isiyo ya kawaida tunayoona kwa sasa kusini-mashariki mwa Australia inaweza kuonyesha hali mbaya ambayo inaweza kuongezeka katika miezi ijayo. "

Nchi inahofia moto kuwa mbaya kama ule wa majira ya joto ya kusini mwa 2019-2020. Mawimbi ya joto ya msimu wa kuchipua yanayoenea mashariki mwa Australia yanafuata majira ya baridi kali zaidi kuwahi kurekodiwa tangu manzo wa rekodi mwaka wa 1910.

(Pamoja na mashirika)

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.