Pata taarifa kuu

China yakosoa ziara ya wabunge wa Ujerumani Taiwan

Wakati Taiwan ikilaani mazoezi ya kivita yaliyofanywa Jumapili Januari 8 na jeshi la China karibu na kisiwa cha Taiwan, Beijing inashutumu, kwa upande wake, kuwasili kwa ujumbe wa wabunge wa Ujerumani huko Taipei.

Uhusiano kati ya Beijing na Taipei umezorota mnamo 2022, Beijing ikiwa imezidisha mazoezi ya kijeshi karibu na kisiwa ambacho inakichukulia kuwa sehemu ya ardhi yake.
Uhusiano kati ya Beijing na Taipei umezorota mnamo 2022, Beijing ikiwa imezidisha mazoezi ya kijeshi karibu na kisiwa ambacho inakichukulia kuwa sehemu ya ardhi yake. AP - Chiang Ying-ying
Matangazo ya kibiashara

"Sababu kuu ya tatizo la Taiwan ni kwamba sheria ya msituni, utawala wa kivita, ukoloni, utawala wa kijeshi na utaifa ulikuwa umeenea duniani, na China iliteseka sana kutokana na hili," amesema msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China katika mkutano na waandishi wa habari. "Ujerumani ilishuhudia somo la kina la kihistoria na lenye uchungu kuhusu suala hili," ameongeza, akilenga ujumbe wa wabunge wa Ujerumani waliowasili Taiwan Jumatatu, Januari 9. "Tunawaomba wanasiasa hawa wa Ujerumani kuzingatia kwa dhati kanuni ya China moja."

Wabunge wa Ujerumani wananuia "kuonyesha mshikamano (wao) na raia wa Taiwan kwa ziara hii", amesema Bi. Strack-Zimmermann, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi ya bunge la Ujerumani (Bundestag). Johannes Vogel, kutoka chama cha kiliberali cha FDP, mwanachama wa muungano wa Kansela Olaf Scholz, alichapisha kwenye Twitter picha yake na mwenzake Marie-Agnes Strack-Zimmermann wakiwa kwenye "ndege kuelekea Taiwan".

"Kwa kuzingatia vitisho vya kijeshi vya China, tumekuja Taiwan kama wajumbe wa FDP, kwa sababu ishara ya msaada kwa Taiwan inahitajika leo," Johannes Vogel ameliambia shirika la habari la AFP. Mbunge huyo wa Ujerumani anabaini kwamba hali inayoikabili Taiwan inatia wasiwasi. Amezungumzia uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine, na kumhusisha Rais wa China Xi Jinping na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin, ambaye alisema pia anaweza kujaribiwa kuanzisha vita. "Baada ya Putin anakuja Xi," Bw. Vogel amesema.

Wabunge wa Ujerumani pia wana wasiwasi kuhusu utegemezi mkubwa wa Ujerumani kwa uchumi wa China, mshirika wake mkubwa zaidi wa kibiashara mnamo 2021.

Wizara ya Ulinzi ya Taiwan imeripoti kuwa ndege 57 za China na meli nne zilifanya mazoezi ya kivita karibu na Taiwan kwa muda wa saa 24 zilizopita. Kati ya ndege hizi, 28 zilipenya eneo la ulinzi wa anga la kisiwa hicho, amesema Jumatatu, Januari 9.

(Pamoja na AFP)

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.