Pata taarifa kuu
USHIRIKIANO-DIPLOMASIA

Nancy Pelosi awasili Taiwan licha ya onyo kutoka Beijing

Baada ya kusababisha sitofahamu kwa muda mrefu katika ziara yake nchini Taiwan, spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani, Nancy Pelosi, aliwasili kisiwani humo Jumanne hii, Agosti 2 jioni. Ziara hiyo inaweza kuchochea uhasama katika uhusiano ambao tayari umeyumba kati ya Washington na Beijing.

Nancy Pelosi (katikati) alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Taipei, Taiwan, tarehe 2 Agosti 2022.
Nancy Pelosi (katikati) alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Taipei, Taiwan, tarehe 2 Agosti 2022. AP
Matangazo ya kibiashara

Nancy Pelosi ndiye afisa wa juu zaidi wa Marekani aliyechaguliwa kutembelea kisiwa hicho kwa kipindi cha miaka 25. Kuwasili kwake kulionyeshwa moja kwa moja kwenye mtandao wa YouTube wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Taiwan. Mkuu wa wabunge wa Marekani alitua Jumanne jioni hii kwenye uwanja wa ndege wa Songshan, ambapo amepokelwa na Joseph Wu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Taiwan.

"Ziara ya wajumbe wetu nchini Taiwan inaheshimu dhamira isiyoyumba ya Marekani ya kuunga mkono demokrasia yenye kudumu ya Taiwan," Nancy Pelosi amesema alipowasili kisiwani humo. "Ziara yetu ni mojawapo ya ziara nyingi za Bunge la Congress nchini Taiwan na haipingani na sera ya muda mrefu ya Marekani. "

"Hatua za kijeshi zinazolengwa"

Beijing imejibu mara moja kwa kushutumu tabia ya "hatari sana" ya Marekani, ambayo inaendelea "kupotosha, kuficha na kufuta maana ya kanuni ya China moja, kuimarisha mawasiliano yake rasmi na Taiwan na kuhimiza shughuli za wanaotaka "kujitenga" nchini Taiwan " . Wizara ya Ulinzi ya China imetangaza "hatua za kijeshi zilizolengwa" ili "kutetea kwa uthabiti uhuru wa kitaifa na uadilifu wa kisiwa hiki".

Mamlaka China, mapema ilionya Washington dhidi ya uwezekano wa ziara ya Nancy Pelosi kwenda Taiwan, ikionya kwamba Marekani "itajutia shambulio lao dhidi ya uhuru na usalama wa China". "Upande wa Marekani umesaliti neno lake kuhusu suala la Taiwan," Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi amesema katika taarifa yake, akimaanisha ahadi ya Marekani, tangu mwaka 1979, ya kutokuwa na uhusiano rasmi na Taiwan.

China inachukulia Taiwan, yenye wakazi wapatao milioni 23, kuwa mojawapo ya majimbo yake ambayo bado haijafanikiwa kuungana tena na maeneo yake mengine tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini China (1949). Ikipinga mpango wowote unaoipa mamlaka ya Taiwan uhalali wa kimataifa, Beijing inapingana na mawasiliano yoyote rasmi kati ya Taiwan na nchi nyingine.

Nancy Pelosi amewasiliTaiwan akitokea Malaysia, hatua ya pili ya ziara yake katika bara la Asia baada ya Singapore. Kwa mujibu wa gazeti la Taiwan la Liberty Times, ambalo linataja vyanzo visivyojulikana, kiongozi huyo wa Marekani anatazamiwa kukutana na Rais wa Taiwan Tsai Ing-wen siku ya Jumatano, adui wa Beijing, kwa sababu anatoka chama kinachotetea uhuru.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.