Pata taarifa kuu
USALAMA-JAMII

Wakristo wa Nigeria waandamana kwa amani baada ya mashambulizi ya Krismasi

Maelfu kadhaa ya Wakristo walikusanyika siku ya Jumatatu katika mji wa Jos, katikati mwa Nigeria, kupinga ukosefu wa usalama baada ya mashambulizi ambayo yalisababisha vifo vya karibu watu 200 katika vijiji jirani wakati wa kipindi cha Krismasi.

Wakristo wakati wa Misa ya Mwaka Mpya.
Wakristo wakati wa Misa ya Mwaka Mpya. © AFP
Matangazo ya kibiashara

Waandamanaji hao wakiwa wamevalia nguo nyeusi kuashiria maombolezo yao walikusanyika mbele ya ofisi ya gavana wa Jimbo la Plateau kudai amani na usalama. Jimbo la Plateau, lililo kwenye mstari wa mpaka kati ya eneo la kaskazini mwa Nigeria lenye Waislamu wengi na eneo la kusini lenye Wakristo wengi, mara kwa mara hukumbwa na milipuko ya vurugu za kidini na kikabila.

"Tunadai bila shaka na kwa msisitizo kukomeshwa kwa mashambulizi haya na mauaji katika jimbo la Plateau na kote nchini," amesema Mchungaji Stephen Baba Panya, mratibu wa maandamano hayo. "Mafisa wa usalama wanapaswa kutumwa katika maeneo mengi ya nchi ili kuzuia kurudiwa kwa mauaji ya Krismasi," ameongeza.

Katika mashambulizi ya mwezi uliopita katika majimbo ya Bokkos na Barkin Ladi, watu wenye silaha walishambulia karibu vijiji 20 siku ya mkesha wa Krismasi na siku zilizofuata, na kuua takriban watu 198, kulingana na mamlaka ya Jimbo la Plateau. Maelfu ya watu pia walikimbia makazi yao wakati wa mashambulizi haya, ambayo yaliathiri zaidi vijiji vya Wakristo.

Takriban watu elfu tano walishiriki katika maandamano ya Jumatatu, wakiwa na mabango yenye maandishi "Sisi ni binadamu, sisi si wanyama" na "Plateau lazima iwe huru", kulingana na mwandishi wa shirika la habari la AFP.

Gavana wa Jimbo la Plateau Caleb Mutfwang alitoa ahadi yake ya kuwafikisha wahusika wa mashambulizi hayo mbele ya sheria. Ingawa serikali mara kwa mara imekuwa eneo la mvutano na vurugu kati ya wakulima na wafugaji wa kuhamahama, mamlaka haijashutumu kundi lolote kwa kuhusika na mashambulizi hayo. Bw Mutfwang amesema ni "ugaidi mtupu".

Siku ya Jumapili muungano wa makundi ya wafugaji wa Kiislamu katika Jimbo la Plateau, unaoongozwa na Muhammad Nura Abdullahi, uliambia mkutano wa wanahabari kwamba zaidi ya wapiganaji wake 30 waliuawa katika mashambulizi hayo. Eneo la Kaskazini-magharibi na katikati mwa Nigeria kwa muda mrefu limekuwa likitishwa na wanamgambo, majambazi ambao wanaendesha operesheni zao kutoka kwenye kambi ndani ya misitu na kuvamia vijiji ili kupora na kuwateka nyara wakazi ili kupata fidia.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.