Pata taarifa kuu
USALAMA-ULINZI

Nigeria: Watu 15 wauawa katika mashambulizi ya wanajihadi wakati wa siku ya Mwaka Mpya

Takriban watu 15 waliuawa katika mashambulizi ya wanajihadi wakati wa siku ya Mwaka Mpya dhidi ya vijiji viwili katika jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria, kulingana na shirika la habari la AFP likinukuu wakazi watatu siku ya Jumatano.

Tangu kuanza kwa uasi wa wanajihadi mwaka 2009, mzozo huo umesababisha vifo vya zaidi ya watu 40,000 na milioni mbili kuyatoroka makazi yao nchini Nigeria, na kusababisha mgogoro mkubwa wa kibinadamu.
Tangu kuanza kwa uasi wa wanajihadi mwaka 2009, mzozo huo umesababisha vifo vya zaidi ya watu 40,000 na milioni mbili kuyatoroka makazi yao nchini Nigeria, na kusababisha mgogoro mkubwa wa kibinadamu. © AFP
Matangazo ya kibiashara

Washambuliaji waliwasili siku ya Jumatatu wakiwa na malori kadhaa yaliyokuwa na bunduki na pikipiki katika vijiji vya Gatamarwa na Tsiha, karibu na mji wa Chibok, wakaazi wamesema. "Idadi ya waliouawa katika mashambulizi hayo katika vijiji hivyo viwili imefikia 15," Manasseh Allen, mkuu wa Chama cha Maendeleo ya Eneo la Chibok (CADA), ameliambia shirika la habari la AFP.

Wanajihadi hao pia walimteka nyara msichana mmoja huko Tsiha, amesema Samson Bulus, mkazi mwingine. Nahum Daso, msemaji wa polisi wa jimbo la Borno, alithibitisha shambulio hilo, lakini hakutoa maelezo wala kutoa idadi ya waliouawa.

Wanajihadi hao, wakiwa wamevalia kama wanajeshi, waliingia Gatamarwa mwendo wa saa 1600 alaasiri, na kuwafyatulia risasi wakazi, ikiwa ni pamoja na kundi la watu waliokuwa wakirejea kutoka kwenye mazishi, Bw Allen amesema. "Waliua watu 12 huko Gatamarwa na wengine watatu huko Tsiha," ameongeza. Idadi iliyothibitishwa na watu wengine wawili.

"Mbali na mauaji, waasi hao walichukua chakula na kuchoma nyumba katika vijiji hivyo viwili," amesema Ayuba Alamson, kiongozi wa raia huko Chibok. Kwa sasa, hakuna ushahidi wa kubainisha wazi kundi la kijihadi lililofanya mashambulizi haya.

Katika eneo hilo, kundi la Kiislamu la Boko Haram na kundi hasimu, Islamic State in West Africa (ISWAP), wote wanafanya mashambulizi dhidi ya wakazi.

Hata leo, mji wa Chibok bado unahusishwa na utekaji nyara wa Boko Haram mwaka wa 2014 wa wasichana zaidi ya 270 wenye umri wa miaka 12 hadi 17, ambao ulizua wimbi kubwa la hasira ya kimataifa na kampeni iliyoitwa #BringBackOurGirls kuwaachilia huru. Takriban nusu yao bado hawajulikani walipo, wengi wao waliolewa kwa lazima na wapiganaji wa kijihadi.

Tangu utekaji nyara huu mkubwa wa wasichana wa shule, hatua za usalama zimeimarishwa katika baadhi ya maeneo ya jimbo hilo, lakini uvamizi mbaya wa makundi ya Kiislamu unaendelea huko.

Tangu kuanza kwa uasi wa wanajihadi mwaka 2009, mzozo huo umesababisha vifo vya zaidi ya watu 40,000 na milioni mbili kuyahama makazi yao nchini Nigeria, na kusababisha mgogoro mkubwa wa kibinadamu, kulingana na Umoja wa Mataifa. Ghasia hizo zimeenea hadi nchi jirani za Niger, Chad na Cameroon.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.