Pata taarifa kuu
ETHIOPIA-USALAMA

Marekani yajaribu kutuliza mgogoro Ethiopia

Wakati mzozo ulioanza katika eneo la Tigray nchini Ethiopia ukitimiza mwaka mmoja, diplomasia ya kimataifa inafanya kazi katika nyanja kadhaa ili kutuliza uhasama huo unaoendelea kati ya waasi na utawala wa Abiy Ahmed.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, katika majengo yake mjini Addis Ababa, Novemba 30, 2020.
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, katika majengo yake mjini Addis Ababa, Novemba 30, 2020. AP - Mulugeta Ayene
Matangazo ya kibiashara

Mjumbe maalum wa Marekani, Jeffrey Feltman, anazuru Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia leo Alhamisi, na rais wa nchi jirani ya Kenya, Uhuru Kenyatta, ametoa wito wa kusitishwa kwa mapigano mara moja.

Vita hivi, ambavyo awali vilihusu jeshi la shirikisho dhidi ya vikosi katika jimbo la Tigray, tayari vimegharimu maisha ya maelfu ya watu na mamilioni ya wengine kuyahama makazi yao tangu mwezi Novemba 2020.

Sasa vita hivi vinatishia kuukumba mji mkuu, Addis Ababa, ambako kunapatikana makao makuu ya Umoja wa Afrika, AU.

Makao makuu ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa.
Makao makuu ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa. RFI/Miguel Martins

Vikosi vya Tigray vimeteka miji muhimu katika siku za hivi karibuni na kuungana na kundi lingine lenye silaha, na kusababisha serikali ya nchi ya pili kwa idadi kubwa ya watu barani Afrika kutangaza hali ya hatari nchi nzima.

Siku ya Jumatano, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema alizungumza na Waziri Mkuu Abiy Ahmed akimsihi kuweka sawa mazingira ya mazungumzo ili mapigano yakome".

Ni vigumu kwa sasa kusema ikiwa njia hii itafanikiwa.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu kwa mara nyingine tena ametoa wito kwa wananchi kuinuka na "kuzika" vikosi vya TPLF. Mtandao wa kijamii wa Facebook ulisema Jumatano ulifuta chapisho kutoka kwa Bw. Abiy, ukibaini kwamba maoni yake yalikuwa yanachochea vurugu.

Kwa upande wao, vikosi vya TPLF, kupitia  msemaji wao Getachew Reda, vimedai katika ujumbe wa Twitter uliochapishwa mwishoni mwa Jumatano kwamba "wameungana" na kundi jingine lenye silaha, Oromo Liberation Army, OLA, kwa kuteka mji wa Kemisse, karibu na Addis Ababa.

Dai hili halikuweza kuthibitishwa kwa wakati huu.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa Jumatano ilibainisha vitendo vya "uhalifu wa kivita" na "uhalifu dhidi ya binadamu", vinavyohusishwa "pande zote", ikiwa ni pamoja na vikosi kutoka nchi jirani ya Eritrea.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.