Sudan yakaribisha tamko la Pompeo kuhusu kuiondoa katika orodha ya ugaidi
Serikali la Sudan imeridhia tamko la waziri wa mashauriano ya kigeni nchini Marekani, Mike Pompeo kuwa serikali ya Khartoum itaondolewa kwenye orodha ya mataifa yanayofadhili ugaidi.
Imechapishwa:
Pompeo kwa zaidi ya mara moja amesema Marekani inanuia kuondoa kikwazo hicho ambacho kimeathiri uwekezaji kwenye nchi ya Sudan, ingawaje mataifa hayo mawili bado yanaafikiana kuhusu fidia inayostahili kulipa wahanga wa shambulio la bomu la mwaka 1998.
Siku ya Alhamisi, Pompeo aliiambia kamati ya bunge la seneti kuhusu uhusiano wa kigeni kwamba sheria kuhusu fidia inapaswa kuwasilishwa mbele ya bunge hivi karibuni.
Uhusiano kati ya nchi hizo mbili ulikuwa umedorora kabisa kwa kipindi cha miaka 30 ya utawala wa Omar al-Bashir, aliyepinduliwa madarakani kufuatia maandamano makubwa.
Tangu mwaka 1993, wakati Rais Bashir alimpokea kiongozi wa mtandao wa al-Qaeda Osama bin Laden, Sudan iliwekwa kwenye orodha nyeusi ya "mataifa yanayounga mkono ugaidi".
Mwaka 1998, baada ya mashambulizi makubwa ya Al-Qaeda dhidi ya balozi za Marekani nchini Kenya na Tanzania, Washington iliendesha mashambuizi ya anga nchini Sudani.