Pata taarifa kuu
DRC-BENI-SIASA-USALAMA

DRC: Kura hewa yapigwa katika mji wa Beni

Raia wa Beni moja ya maeneo ambayo uchaguzi umeahirishwa hadi mwezi Machi mwaka 2019 wamepiga kura hewa ili kupinga uamuzi wa Tume ya Uchaguzi nchini DRC (CENI) kuahirisha uchaguzi katika maeneo matatu ya nchi hiyo Beni, Butembo na Yumbi, Magharibi mwa nchi.

Watu waliokuwa wakisubiri kupiga kura waandamana mbele ya kituo cha kupiga kura katika Chuo cha St Raphael mjini Kinshasa Desemba 30, 2018.
Watu waliokuwa wakisubiri kupiga kura waandamana mbele ya kituo cha kupiga kura katika Chuo cha St Raphael mjini Kinshasa Desemba 30, 2018. Luis TATO / AFP
Matangazo ya kibiashara

Mashirika ya vijana na wakazi wa Beni wametenga vituo kadhaa vya kupiga kura na wakazi wa mji huo waliitikia wito wa mashirika hayo kuja kupiga kura.

Mapema wiki hii, Tume ya Uchaguzi (CENI) katika taarifa yake imesema, sababu ya uchaguzi huo kuahirishwa hadi mwezi Machi mwaka 2019, ni kwa sababu ya changamoto za kiusalama katika maeneo hayo ambayo yameendelea kushuhudia mashambulizi ya makundi ya waasi.

Kabla ya kutolewa kwa tangazo hili, Tume ya Uchaguzi ilionesha wasiwasi wake kuhusu usalama wa wafanyikazi na vifaa vya kupigia kura katika Wilaya ya Beni, ambayo wakaazi wameendelea kusumbuliwa na waasi wa ADF NALU.

Wiki mbili zilizopita, ghala la kuhifadhi vifaa vya kupigia kura, pia viliteketea moto katika wilaya ya Beni.

Hivi karibuni watu watano waliuawa baada ya kushambuliwa na waasi wa ADF, na kuzua wasiwasi wa iwapo Uchaguzi huo utafanyika katika eneo hilo ambalo pia linasumbuliwa na maambukizi ya ugonjwa hatari wa Ebola.

Wapiga kura milioni 40 wanashiriki uchaguzi huo. Tume ya Uchaguzi inasema, mshindi atatangazwa tarehe 15 na kuapishwa tarehe 18 mwezi Januari.

Hakuna duru ya pili ya Uchaguzi nchini DRC, anayeshinda atatangazwa na Tume hiyo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.