Pata taarifa kuu
BURUNDI-USALAMA-SIASA

Burundi: Rais Nkurunziza atoa kauli ya mwisho kwa wapiganaji

Katika hutuba yake kwa taifa katika lugha ya Kirundi, lugha ya taifa ya Burundi, Jumatatu wiki hii, Rais Pierre Nkurunziza ametoa siku tano kwa wananchi wenzake waliolazimika kuchukua silaha na kuchukuliwa kama"wahalifu wenye silaha".

Rais Pierre Nkurunziza amewaahidi wale ambao walichukua silaha kuwa hawatafunguliwa mashitaka kama watajisalimisha ndani ya siku tano.
Rais Pierre Nkurunziza amewaahidi wale ambao walichukua silaha kuwa hawatafunguliwa mashitaka kama watajisalimisha ndani ya siku tano. AFP PHOTO / LANDRY NSHIMIYE
Matangazo ya kibiashara

Viongozi wa Burundi wanalinyooshea kidole kundi la waasi lililoundwa mwishoni mwa mwezi Aprili baada ya kupinga Rais Pierre Nkurunziza kuwania muhula wa tatu. Katika hotuba yake, Rais Nkurunziza pia ametoa wito kwa mazungumzo ya kitaifa, ambayo amesema yatafanyika nchini Burundi.

Kwa jumuiya ya kimataifa ambayo imekua ikimshinikiza juu ya kuandaa mashauriano ya kitaifa na wapinzani wake wote, Rais Nkurunziza ameonekana kupuuzia jambo hilo. Ametolea wito raia wake " kujiandaa kwa ajili ya mjadala wa kitaifa, lakini utakaofanyika nchini ". kauli hii ya Rais Nkurunziza inaonyesha kuutenga upinzani ulio uhamishoni kushiriki katika mazungumzo hayo.

Pierre Nkurunziza ameonya na kutoa muda wa siku tano kwa makundi ya watu wanaomiliki silaha kuwa wamerejesha silaha hizo kwa vyombo husika, la sivyo watakiona cha mtimakuni.

Si mara ya kwanza Nkurunzia anatoa kauli kama hiyo. Mwezi uliyopita wa Septemba Pierre Nkurunziza alisema akisisitiza kuwa yoyote yule anayemiliki silaha kinyume cha sheria, ambaye atakua hajarejesha silaha ndani ya kipindi cha miezi miwili atajuta. Lakini zoezi hilo linaonekana kuwa halikufanyika, kwani baada ya kauli hiyo, mashambulizi ya hapa na pale yameendelea kuripotiwa kwa wingi hadi leo, Usiku wa Jumapili kuamkia Jumatatu wiki hii, watu zaidi ya watano wameuawa katika baa moja linalojulikana kwa jina la Watsapp wilayani Bwiza mjini kati Bujumbura, huku mwili wa mwanaume ukiokotwa mbele ya ofisi ya mkuu wa wilaya ya Musaga, kusini mwa jiji la Bujumbura. Mwili wa mwanamke ia uliokotwa usiku wa Jumapili kuamkia Jumatatu eiki hii katika eneo la Gikungu, wilayani Gihosha kaskazini mashariki mwa jiji la Bujumbura.

Mjini Bujumbura na vitongoji vyake, miili ya watu imekua ikiokotwa kila kukicha.

Jumamosi Oktoba 31, zaidi ya watu 16 kwa mujibu wa mashahidi, waliuawa na polisi kijijini Buringa wakati walipokua wakitokea wilayani Mpanda, mkoani Bubanza kwenye mazishi ya kijana mmoja, mkazi wa wilaya Cibitoke. hata hivyo msemaji wa polisi Pierre Nkurikiye alisema kuwa mtu mmoja ndie aliye uawa, huku akibaini kuwa watu hao walikutwa na silaha katika magari yao. Madai ambayo yalikanushwa na wakazi wa kijiji cha Buringa.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.