Pata taarifa kuu
BURUNDI-BUYOYA-HAKI

Pierre Buyoya: Siogopi kusafirishwa na nchi yoyote kujibu mashitaka yanayonikabili Burundi

Rais wa zamani wa Burundi Pierre Buyoya, anayekabiliwa na mashitaka ya mauaji ya rais wa kwanza wa Burundi kutoka kabila la Wahutu Melchior Ndadaye mnamo mwaka 1993, anasema haogopi kusafirishwa nchini Burundi kujibu mashitaka yanayomkabili.

Rais wa zamani wa Ireland Mary Robinson (kushoto) na rais wa zamani wa Burundi Pierre Buyoya na mkewe Sophie Buyoya Kigali Aprili 7, 2014.
Rais wa zamani wa Ireland Mary Robinson (kushoto) na rais wa zamani wa Burundi Pierre Buyoya na mkewe Sophie Buyoya Kigali Aprili 7, 2014. © REUTERS
Matangazo ya kibiashara

Hivi karibuni vyombo vya sheria nchini Burundi vilitoa waranti wa kumkamata rais huyo wa zamani aliyechukuwa madaraka kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 1987 kupitia jaribio la mapinduzi ya kijeshi dhidi ya mtangulizi wake Jean Baptiste Bagaza kutoka kabila la Watutsi.

"Sina hofu ya kusafirishwa na Mali au na nchi yoyote kwenda Burundi," amesema Pierre Buyoya, mwakilishi wa sasa wa Umoja wa Afrika nchini Mali, wakati wa mkutano wa waandishi wa habari katika mji mkuu wa Bamako.

"Leo, ukizingatia rekodi ya Serikali ya Burundi katika suala la haki za binadamu, ni vigumu kuamini kwamba vyombo vya sheria nchini humo vinatekeleza majukumu yake au sheria inafuata mkondo wake, na hukumu zote zilizotolewa zinaonyesha kwamba uwezo huu haupo, "ameongeza Bw Buyoya.

Siku ya Ijumaa Burundi ilitoa waranti wa kumkamata Pierre Buyoya, pamoja na maafisa wa zamani 11(jeshi na polisi) na washirika wake watano wa zamani, kwa madai kuhusika katika mauaji ya Melchior Ndadaye.

Hivi karibuni Bw Buyoya alipinga vikali madai kuwa alihusika kwenye kifo cha Bw Ndadaye.

Buyoya amesema katika taarifa kuwa "Kila kitu kinaonesha kuwa huo ni mpango wa kisiasa unaolenga kumchafua na ni mwelekeo mpya wenye lengo la kusahaulisha maumivu ya masuala ambayo bado hayajapatiwa suluhu tangu kuanza kwa mgogoro wa kisiasa nchini humo mwaka 2015.

Tayari maafisa kadhaa wa zamani wa jeshi la Burundi (Ex FAB) wamekamatwa na wengine wanaendelea kutafutwa, huku mali zao nchini zikizuliwa.

Kuuliwa kwa Melchior Ndadaye kulisababisha kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe. Zaidi ya watu 300,000 waliuawa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya jeshi lenye watutsi walio wachache na waasi wa Kihutu vilivyodumu miaka 12. Wakati huo maelfu ya watu walilazimika kutoroka makazi yao na kukimbili nchi jirani.

Kuna hofu kuwa kumlenga Bw Buyoya ambaye ni kutoka kabila la Watutsi anayeishi nchini Mali kunaweza kuchangia kuzuka misukosuko ya kikabila.

Bw Buyoya ambaye alitwaa madaraka mara mbili ndani ya miongo mitatu iliyopita kwa msaada wa jeshi ni mwanadiplomasia anayeheshimiwa barani Afrika.

Buyoya 69, alihusika kwenye mchakato wa amani uliomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe na kuongoza kuchaguliwa kiongozi wa zamani wa waasi wa Hutu Pierre Nkurunziza kuwa rais mwaka 2005.

Wadadisi wanasema hatua ya utawala wa Nkurunziza kutoa waranti wa kimataifa wa kumkamata Pierre Buyoya inalenga kupotosha jumuiya ya kimataifa kwa hali inayojiri nchini humo, ikiwa ni pamoja na kukataa kushiiki mazungumo, ukiukwaji wa haki za binadamu unaoendelea nchini humo.

Mapem awiki hii Umoja wa Afrika uliionya Burundi dhidi ya hatua zinazoweza kuhujumu mchakato wa amani baada ya kutolewa waranti wa kimataifa wa kumkamata rais wa zamani Pierre Buyoya na maafisa wengine 16.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.