Pata taarifa kuu
BRAZIL-TANZIA

Salamu za maombolezo zaendelea kutolewa kufuatia kifo cha nguli za soka Pele

Mashabiki wa soka, wadau wa michezo na viongozi wa dunia, wameendelea kutoa salamu za maombolezo kwa nchi ya Brazil na familia ya mwanasoka nyota wa zamani, Pele, ambaye alifariki dunia jana akiwa na umri wa miaka 82.Β 

Pele,Mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Brazil
Pele,Mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Brazil AFP
Matangazo ya kibiashara

Jina lake halisi ni Edson Arantes do Nascimento, lakini kutokana na umahiri wake uwanjani na mafanikio aliyoipatia nchi yake, mashabiki walimpa jina la utani kama Pele.Β 

Akiwa na umri wa miaka 17 pekee, Pele aliisaidia nchi yake kutwaa taji la kombe la dunia mwaka 1958 nchini Sweden, akitajwa kama mchezaji aliyeweka rekodi ya dunia kwa kufunga magoli 1281 katika michezo 1363, ikiwemo magoli 77 katika mechi 92 alizochezea timu yake ya taifa.Β 

Aidha Pele ndie mchezaji pekee duniani hadi sasa kufanikiwa kushinda mara tatu taji la kombe la dunia mwaka 1958, 1962 na 1970, huku mwaka 2000 akitajwa na shirikisho la soka duniani FIFA kama mchezaji bora wa karne.Β 

Kwa muda mrefu Pele alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya figo na saratani ya kibofu cha mkojo, ambapo mwaka 2021 alifanyiwa upasuaji mjini Sao Paulo kuondoa saratani hiyo kabla ya kurejea tena hospitali mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka huu.Β 

Shughuli za mazishi zinatarajiwa kufanywa nje kidogo ya jiji la Sao Paulo katika uwanja wa Vila Belmiro, uwanja ambao Pele aliutumia kucheza akiwa na klabu yake ya Santos, huku jeneza lake likitarajiwa kupitishwa mbele ya nyumba ya mama yake Celeste Arantes mwenye umri wa miaka 100 siku ya Jumanne.Β 

Wachazaji nguli barani Afrika na duniani akiwemo Samuel Etoo, Michael Essien na wengine wengi, waliandika ujumbe kumsifu na kutoa pole kwa familia yao ama kuchapisha picha wakiwa na Pele.Β 

Kwa mashabiki wa Soka, Edson Arantes do Nascimento maarufu kama Pele, atabakia kuwa mmoja ya wachezaji ambao waliufanya mpira wa miguu kupendwa pamoja na kuleta umoja nchini mwake, akipata umaarufu mkubwa barani Afrika.Β 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.