Sumgong aweka historia kwa kuishindia Kenya medali ya dhahabu mbio za Marathon
Mwanariadha Jemima Sumgong kutoka nchini Kenya, ameishindia nchi yake medali ya kwanza ya dhahabu katika historia ya mbio za Marathon katika Michezo ya Olimpiki kwa upande wa wanawake.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Sumgong amemaliza mbio hizo kwa muda wa saa 2 dakika 24 na sekunde 04, akifuatwa na Eunice Jepkirui Kirwa raia wa Bahrain, ambaye alibadilisha uraia wake kutoka nchini Kenya mwaka 2013.
Bingwa wa dunia wa mbio hizi, Mwiethiopia Mare Dibaba, naye alimaliza wa tatu.
Sumgong ataendelea kukumbukwa katika siku zijazo kwa kuwa Mkenya wa kwanza kupata medali ya dhahabu katika mbio hizi za Kilomita 42 katika michezo hii ya Olimpiki inayoendelea nchini Brazil.
Wakenya wengine kama Catherine Ndereba na Prisca Jeptoo, katika miaka iliyopita wamekuwa wakijaribu kupata medali ya dhahabu bila mafanikio.
Kuelekea katika michezo hii, Sumgong mwenye umri wa miaka 31, alishinda mashindano ya London Marathon mwezi Aprili mwaka huu.