Pata taarifa kuu
OLIMPIKI-BRAZIL 2016

WADA yasikitishwa na IOC kwa kutoifungia Urusi

Shirika la kupambana na matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku kwa wanamichezo duniani WADA, linasema limesikitishwa sana na uamuzi wa Kamati ya Kimataifa ya Michezo ya Olimpiki IOC kutoifungia Urusi kushiriki katika Michezo ya Olimpiki itakayoanza tarehe 5 mwezi ujao nchini Brazil.

Makao makuu ya Shirika la WADA nchini Canada
Makao makuu ya Shirika la WADA nchini Canada REUTERS/Christinne Muschi
Matangazo ya kibiashara

WADA yenye makao yake mjini Montreal nchini Canada, imesema itaendelea kuhakikisha kuwa wanamichezo hawatumii dawa zilizopigwa marufuku kushinda michezo mbalimbali wakati wa mashindano hayo na mengine ya kimataifa.

Shirika hilo limekuwa likisema kuwa lilikuwa na ushahidi kuwa, wachezaji wengi wa Urusi hasa wanariadha walikuwa wametumia dawa za kuwaongezea nguvu mwilini wakati wa mashindano mbalimbali ya kimataifa.

Kabla ya uamuzi huo, WADA ilikuwa imeiomba IOC kuwapiga marufuku wanariadha wote wa Urusi waliotajwa kutumia dawa zilizopigwa marufuku, kutoshiriki katika Michezo hiyo.

Australia kupitia Waziri wake wa Michezo Sussan Ley naye ameshtumu uamuzi huo wa IOC kwa kile alichokisema, uamuzi huo unatia doa michezo hiyo ya Olimpiki.

Hata hivyo, IOC mwishoni mwa juma lililopita iliamua kuwa haitaipiga marufuku Urusi kushiriki katika michezo ya Olimpiki lakini ikavitaka vyama vya michezo nchini humo kuhakikisha kuwa vinawapima wachezaji wote watakaoshiriki katika michezo hiyo.

Serikali ya Urusi imepongeza uamuzi huo wa IOC na kusema ulikuwa wa haki.

Urusi inatarajiwa kutuma zaidi ya wanamichezo wake 300 kushiriki katika michezo mbalimbali katika mashindano hayo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.