Pata taarifa kuu
TANZANIA-SOKA-COSAFA

Tanzania yaelemewa michuano ya COSAFA

Timu ya taifa ya soka ya Tanzania, Taifa Stars imebanduliwa nje ya michuano ya COSAFA kuwania taji la kusini mwa nchi za Afrika baada ya kufungwa na Madagascar mabao 2 kwa 0 Jumatano usiku wiki hii.

Mashabiki wa Taifa Stars wakati ilipokua ikifuana na Cote d'Ivoire  June 16 mwaka 2013.
Mashabiki wa Taifa Stars wakati ilipokua ikifuana na Cote d'Ivoire June 16 mwaka 2013. YouTube
Matangazo ya kibiashara

Tanzania imepoteza mchuano wake wa pili katika michuano hiyo baada ya kufungwa na Swaziland katika mchuano wa ufunguzi kwa bao 1 kwa 0.

Madagascar ilipata mabao yake katika dakika ya 14 kupitia mchezaji Rakotoharimalala huku Randrianmanjaka akifunga la pili katika dakika 44 ya kipindi hicho dakika moja kabla ya mapumziko.

Mashabiki wa soka nchini Tanzania wamesikitishwa na matokeo hayo hasa kwa kufungwa na Madagascar na Swaziland ambazo zipo chini yake katika orodha ya Shirikisho la soka duniani FIFA.

Mwenyekiti wa Shirikisho la soka nchini Tanzania TFF Jamal Malinzi amesema licha ya kusikitishwa na matokeo hayo, sio mwisho wa soka nchini humo.

“ Kuvunjika koleo sio mwisho wa uhunzi ”, Jamal Malinzi amenukuliwa katika ukurasa wake wa Twitter.

Vijana wa Stars chini ya kocha Mholanzi Mart Nooij wanasubiri sasa mchuano wake wa mwisho dhidi ya Lesotho kesho Ijumaa kabla ya kurudi jijini Dar es salaam.

Wachambuzi wa soka wanasema huenda TFF ikamchukulia hatua kocha Nooij kwa kushindwa kufanya vizuri katika michuano hiyo.

Katika matokeo mengine, Swaziland waliwashinda Lesotho mabao 2 kwa 0 na kundi hilo linaoongozwa na Madagascar kwa alama 6 sawa na Swaziland lakini Lesotho na Tanzania hazina alama yoyote.

Michuano ya mwisho ya kundi la A inachezwa leo Alhamisi na mshindi kati ya Zimbabwe na Namibia atafuzu katika hatua ya robo fainali lakini Ushelisheli inaweza kufuzu ikiwa itapata ushindi wa mabao mengi dhidi ya Mauritius ikiwa Zimbabwe itawashinda Namibia.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.