Kenya: Mahakama imetupilia mbali sheria kuhusu kodi ya makaazi
Mahakama nchini Kenya, imefuta sheria kuhusu kodi ya makaazi, ikisema ni kinyume cha Katiba, uamuzi ambao ni pigo kwa serikali ya rais Ruto ambayo kwa mujibu wake inajaribu kuliondoa taifa hilo kwenye changamoto za kiuchumi.
Imechapishwa:
Hatua hii imekuja baada ya serikali mwezi Juni, kuanza kuwakata wafanyakazi asilimia 1.5 ya mshahara wao kila mwezi ili kufadhili mpango wake wa ujenzi wa makaazi ya bei nafuu.
Aidha mwajiri pia amekuwa akimlipia mfanyakazi wake asilimia 1.5 ya mshahara, kufanikisha mpango huo
Jopo la majaji watatu wa mahakama kuu jijini Nairobi katika uamuzi wake limesema mpango huo haukufuata sheria kabla ya utekelezwaji wake ambapo pia haukuwajumuisha wafanyikazi katika sekta zote, suala ambalo wamelitaja kuwa la kibaguzi.
Kwa mujibu wa jaji wa mahakama hiyo, Jaji David Majanja, serikali kupitia mamlaka ya utozaji ushuru KRA, imezuiliwa kukusanya kodi hiyo ya makaazi.
Kodi hiyo ilikuwa sehemu ya sheria ya kifedha ya mwaka wa 2023, iliyoongeza ushuru kwa baadhi ya bidhaa, hali ambayo imeonekana kuwa mzigo kwa raia wa taifa hilo ambao tayari wanakabiliwa na mfuko wa bei za bidhaa.
Breaking: High Court declares Housing Levy unconstitutional, says it lacks a comprehensive legal framework #FinanceAct2023 pic.twitter.com/us3DsEK0V3
— Citizen TV Kenya (@citizentvkenya) November 28, 2023
Ghadhabu iliyotokana na hatua hiyo ya kupanda wa bei za bidhaa muhimu haswa chakula na mafuta, ilisababisha kutokea kwa maandamano dhidi ya utawala wa rais Ruto mapema mwaka huu.
Licha ya kukashifiwa, mkuu wa nchi ameteta mpango wa kutoza kodi ya makaazi kwa raia kwa madai kuwa utasaidia kuwajengea raia wake makazi bora pamoja na kutengeneza ajira na kupunguza ukopaji.
Wakosoaji wa rais Ruto wanamtuhumu kwa kwenda kinyume na kutozingatia ahadi alizozitoa kwa wapiga kura kuelekea uchaguzi mkuu wa mwezi Agosti mwaka wa 2022.