Pata taarifa kuu
SIASA-USALAMA

Burundi: Chama cha upinzani cha National Congress for Freedom chakumbwa na mgogoro wa uongozi

Nchini Burundi, chama kikuu cha upinzani bado kinakabiliwa na mgogoro wa uongozi. Kundi linaloundwa na makada kumi, wabunge ambao ni wanachama wa ofisi ya kisiasa wamekuwa wakipinga kwa miezi kadhaa uongozi wa Agathon Rwasa, mpinzani wa kihistoria wa anayeongoza Chama cha kitaifa cha Uhuru (CNL). Wamepiga hatua mpya tangu jana katika pambano kati yao kwa kutangaza kuwa wamemtimua mkuu wa chama. 

Agathon Rwasa, kiongozi wa chama cha upinzani cha National Congress for Freedom,CNL, Mei 20, 2020.
Agathon Rwasa, kiongozi wa chama cha upinzani cha National Congress for Freedom,CNL, Mei 20, 2020. © ONESPHORE NIBIGIRA / AFP
Matangazo ya kibiashara

Wapinzani hao kumi wamethibitisha katika taarifa yao kwa vyombo vya habari kwamba wamemsimamisha kazi kiongozi wa kihistoria wa CNL, Agathon Rwasa, kama rais na mwakilishi wa kisheria, kabla ya kumtaka Katibu Mkuu wa sasa wa chama hiki, Simon Bizimungu, kukaimu nafasi hiyo.

Hata  hivyo Agathon Rwasa amefutilia mbali tangazo hilo akisema kwamba yeye bado ni kiongozi wa chama cha CNL, akitaja uamuzi uliotangazwa 'kichekesho'.

Simon Bizimungu pia anakanusha neno "mgogoro ndani ya chama cha CNL", linalotumiwa na vyombo vya habari kuelezea kinachoendelea.

Simon Bizimungu anabaini kuwa ni "kundi dogo lililojitenga, lisilo na uungwaji mkono wowote wa watu, na ambalo limetengwa rasmi kutoka kwa ofisi ya kisiasa ya CNL".

Tatizo pekee kwa mujibu wake ni uungwaji mkono wanaoupata kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Martin Niteretse, ambaye ameamua kusimamisha shughuli zote za chama cha CNL kwa muda wa mwezi mmoja ilimradi Agathon Rwasa asifikie mwafaka na wapinzani hawa.

Agathon Rwasa hadi sasa amekataa kutii amri hii, akishutumu "uingiliaji usiovumilika wa serikali katika masuala ya ndani" ya chama chake.

Wakati huo huo, shughuli za chama kikuu cha upinzani zimezorota kabisa, ikiwa imesalia mwaka mmoja tu kabla ya uchaguzi wa wabunge nchini Burundi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.