Pata taarifa kuu

WFP:Watu zaidi ya Milioni 24 wako katika hatari ya kukabiliwa na njaa

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani mapema leo limesema  kwamba kupungua kwa ufadhili kumelazimisha kupunguza kwa kiasi kikubwa mgao katika mataifa mengi , likionya kwamba watu milioni 24 huenda wakakumbwa na uhaba wa chakula.

Mwanamme akibeba mfuko wa unga wa mahindi katika kituo cha usambazaji chakula kinachoendeshwa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab, Kenya
Mwanamme akibeba mfuko wa unga wa mahindi katika kituo cha usambazaji chakula kinachoendeshwa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab, Kenya AP - Brian Inganga
Matangazo ya kibiashara

Shirika hilo  limesema limekuwa likijitahidi kukidhi mahitaji ya kimataifa ya msaada wa chakula huku likikabiliwa na upungufu wa ufadhili wa zaidi ya asilimia 60 mwaka huu na ambao ni wa juu zaidi katika historia yake.

"Kwa mara ya kwanza kabisa, WFP imeona michango ikipungua huku mahitaji yakiongezeka,"ilisema WFP katika taarifa yake.

Hii inaweza kuwa na matokeo mabaya, na wataalam wa WFP wanakadiria kuwa kwa kila asilimia moja ya kupunguzwa kwa msaada wa chakula, zaidi ya watu 400,000 wana hatari ya kuangukia katika viwango vya dharura vya njaa.

Kwa kuzingatia upunguzaji mkubwa unaolazimika kufanya, WFP ilionya katika taarifa kwamba "watu zaidi ya milioni 24 wanaweza kutumbukia kwenye njaa ya dharura katika kipindi cha miezi 12 ijayo, ongezeko la asilimia 50 katika kiwango cha sasa.

Mkuu wa WFP Cindy McCain amesema ufadhili zaidi ni muhimu.

Kama hatutapokea usaidizi tunaohitaji ili kuepusha maafa zaidi, dunia bila shaka itaona migogoro zaidi, machafuko zaidi na njaa zaidi,"alisema katika taarifa yake.

Ama tunachochea moto wa kukosekana kwa utulivu duniani, au tunafanya kazi haraka kuzima moto huo.

WFP inakadiria kuwa watu milioni 345 duniani kote wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, katika ngazi ya tatu au zaidi katika uainishaji wa Umoja wa Mataifa wa viwango vitano vya uhaba wa chakula, unaojulikana kama IPC.

Milioni 40 kamili kati yao kwa sasa wanachukuliwa kuwa katika viwango vya dharura vya njaa, au IPC level 4, ikimaanisha wanalazimika kuchukua hatua za kukata tamaa ili kuishi na wako katika hatari ya kufa kutokana na utapiamlo.

"Msaada wa chakula wa shirila la WFP ni njia muhimu ya maisha, mara nyingi ndicho kitu pekee kinachowatenganisha na njaa," ilisema.

Nchini Afghanistan, ambako nusu ya watu wana uhaba wa chakula, WFP kwa mfano ililazimishwa mwezi Mei kupunguza msaada wake kwa asilimia 66, ikimaanisha kwamba watu milioni nane wanaohitaji msaada hawapati tena msaada huo.

Na mwezi Julai, asilimia 45 ya waliopokea misaada nchini Syria na robo ya wale walio kwenye orodha ya WFP nchini Haiti walikatishwa misaada.

WFP ilisema pia ililazimika kupunguza karibu nusu ya mzigo wake nchini Somalia, na kuathiri watu milioni 4.7, katika kilele cha mwitikio wa njaa mwaka jana.

Wataalamu wa shirika la chakula la Umoja wa Mataifa sasa wanahofia kwamba vifo zaidi vitachochewa na hali hiyo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.