Brics kuongeza uanachama wake hadi 11 mwaka ujao
Nairobi – Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ametangaza kuwa muungano wa BRICS utawasajili wanachama wapya sita mwanzoni mwa mwaka ujao.
Imechapishwa:
Iran, Argentina, Misir, Ethiopia, Saudi Arabia na Milki ya falme za kiarabu zitakuwa zinajiunga na muungano huo kuanzia tarehe moja ya mwezi Januari mwaka ujao kwa mujibu wa kiongozi huyo wa Afrika Kusini.
Mjadala wa kuhusu upanuzi wa muungano huo unaojumuisha nchi za Brazil, Urusi, India , China na Afrika kusini, umetawala agenda ya kikao kilichofanyika jijini Johannesburg.
Kwa mujibu wa watu wa karibu na kikao hicho, hakujakuwa na tofauti zozote baina ya wanachama kuhusu upanuzi wa uanachama, mpango ambao umetajwa kuwa mwelekeo bora kutoka kwa mataifa wanachama.
Wachambuzi wa mambo ya kimataifa wanaona kuwa Brics inalenga kupata ushawishi na uungwaji mkono duniani kote.
Idadi kubwa ya mataifa yalikuwa yametuma maombi rasmi ya kujiunga na Brics, ambayo inawakilisha robo ya uchumi wa dunia na zaidi ya watu bilioni tatu.
Baadhi ya wakuu wengine 50 wa nchi na serikali wanahudhuria mkutano huo mjini Johannesburg, ambao unakamilika siku ya Alhamisi.